Msuva apanda dau Morocco
Simon Msuva ni kiungo mshambuliji wa timu ya Diffaa Al Jadida ya nchini Morocco ambaye ametua katika klabu hiyo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Yanga.
Msuva ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Kitanzania wanaowakilisha nchi nje ya nchi wakicheza soka la kulipwa ambapo ameonyesha uwezo wa hali ya juu katika katika klabu yake hiyo kutokana na ubora wake katika kuzoea mazingira mapema na kuwa mfungaji mzuri.
Alijiunga na Al Jadida, Julai 29, mwaka jana kwa dau la dola 150,000 ambalo ni zaidi Sh milioni 337 akitokea Yanga lakini kwa sasa Waarabu wamemthaminisha kwa euro 475,000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.3.
Moja ya mikakati yake ni kuona anafanikiwa kusonga mbele zaidi ili aweze kumfikia Mtanzania mwenzake, Mbwana Samatta anayekipiga katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
Championi ilifanya mazungumzo na kiungo huyo ambaye ameelezea mikakati yake pamoja na kupanda kwa thamani yake kwa sasa.
Mazungumzo hayo ilikuwa ni baada ya mchezo wa Taifa Stars dhidi ya DR Congo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo Msuva alipata nafasi ya kucheza na kuonyesha uwezo mzuri.
UNAZUNGUMZIAJE MCHEZO DHIDI YA DRC?
“Tunashukuru Mungu kwa matokeo tuliyoyapata, tumepoteza mchezo wetu dhidi ya Algeria lakini kuna kitu fulani tumejifunza kutoka kwao, tukicheza mechi nyingi inatusaidia kutuweka vizuri.
“DRC Congo wana timu nzuri ukiangalia mchezaji mmoja mmoja ni tofauti na tulivyo sisi lakini katika mpira lolote linaweza kutokea.
“Mpira unachezeka uwanjani na matokeo yanapatikana uwanjani, tulihamasishana wenyewe kwa wenyewe tuweze kuonyesha kitu na kweli tumefanikiwa kuonyesha kile ambacho Watanzania wanakihitaji.
“Tuliingia uwanjani kama timu, makocha walituhamasisha, manahodha pamoja na wachezaji kwa ujumla tulijipanga ili kuhakikisha tunafanikiwa kufanya vyema na kweli matunda yameonekana kwa kupata ushindi.
UNAZUNGUMZIAJE SAPOTI YA MASHABIKI?
“Naomba mashabiki waiamini timu yao, shabiki kazi yake ni kushangilia timu yake, watambue kwamba timu ni hiihii hakuna tofauti, naamini tutafanya vizuri, waendelee kutupa sapoti ili tufanye vyema, wenzetu nje mashabiki wanashangilia timu yao hata wakifungwa.
KUCHEZA LIGI YA MABINGWA UKIWA NA TIMU YA MOROCCO, INA MAANA GANI KWAKO?
“Ni furaha kwangu, ni mara yangu ya kwanza kucheza mashindano hayo nikiwa Morocco, ninafanya kazi na timu yangu kwa kushirikina na wenzangu, nahitaji kupita njia ya Samatta ili nipate mafanikio makubwa.
UNA MABAO MANGAPI HADI SASA?
“Katika Ligi ya Mabingwa nina mabao manne katika Ligi Kuu ya Morocco nina sita, siyo mwendo mbaya kwangu.
MOROCCO WANAMCHUKULIAJE MSUVA?
“Wamenieleza kuwa mimi ndiyo Mtanzania wa kwanza kuonyesha kiwango kizuri kama changu katika ligi yao, nimefika na kuonyesha mabadiliko ya haraka ndani ya muda mfupi, wananikubali sana. Nimekopi vitu vyao mapema kutokana na kujitambua.
KIPI KILIKUFANYA UZOEE MAPEMA?
“Ligi yao haina tofauti sana na ligi ya Bongo kikubwa ni ushindani tu, niweweza kukutana na watu wanaojua mpira na ndiyo maana nimebadilika kwa haraka, mwalimu amenitengeneza na kunibadilisha, nimekuwa na uwezo mzuri wa kucheza katikati na hata mechi ya Stars na Congo nimecheza kati.
UNAZUNGUMZIAJE KUPANDA THAMANI YAKO?
“(Kumbuka thamani yake ya dau la usajili imepanda na sasa ni Sh bilioni 1.3) Namshukuru Mungu kuona thamani yangu inaendelea kupanda siku hadi siku, kikubwa ninamshukuru Mungu na kila kitu kinawezekana kupitia yeye, nitaendelea kupambana ili nisonge mbele.”
Post a Comment