RC MALIMA AWATAKA WATAALAMU WA AFYA KUWA NA MIKAKATI YA KUBORESHA VIWANGO VYA JUU VYA HUDUMA YA AFYA VINAVYOKIDHI MATARAJIO YA WANANCHI
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, amewataka watoa huduma za afya Mkoa wa Morogoro kuanzia ngazi ya jamii mpaka Hospitali ya Rufaa kuweka mikakati ya kutoa huduma bora na zinazokidhi matarajio ya wananchi kwa wakati kwa kutumia lugha yenye staha na unyenyekevu kitu kitakachowafanya waone matunda ya uwekezaji wa Serikali yao.
Wito huo ameutoa Januari 5/2024 wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo Manispaa ya Morogoro akiwa katika mradi wa ujenzi wa Hopsitali ya Manispaailiyoko Kata ya Kihonda .
RC Malima,amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa ambao umehusisha ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, hospitali za wilaya, Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Rufaa za Kanda, kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa, ununuzi wa vifaa tiba na kuajiri watalaamu wenye weledi wa kada mbalimbali za afya.
Aidha,amesema kuwa Wananchi wanategemea huduma bora wanapofika hospitalini kupata huduma za afya kwani serikali imetekeleza wajibu wake kwa kuboresha miundombinu na kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana katika hospitali zote
“Niwapongeze sana viongozi kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imekuwa ikijivunia huduma zenu, hizi hospitali ndio taswira ya taifa katika utoaji wa huduma hivyo ninyi mkifanya vibaya mnaharibu taswira ya Mkoa mzima katika sekta ya afya " Amesema RC Malima.
Vile vile, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kuzijengea uwezo Vituo vya afya na Zahanati pamoja na kujua taarifa zote muhimu katika miradi ya afya .
Hata hivyo, RC Malima, ametoa rai kwa wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya pale wanapopewa maelekezo kwa kuwa wataalamu hao wana weledi wa kutosha na ushauri wao huwa unazingatia taratibu za kiafya.
Post a Comment