Header Ads

WANANCHI MKOA WA MOROGORO WATAHADHARISHWA NA MAGONJWA YA MLIPUKO.


WANANCHI wa Mkoa wa Morogoro wamekumbushwa kuzingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari ili kuweza kujikinga na magonjwa ya mlipuko kufuatia kuanza kunyesha kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Morogoro  na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.

Tahadhari hiyo imetolewa Januari 17/2024 na Afisa Afya Mkoa wa Morogoro, Bi. Prisca Gallet,  wakati wa kukabidhi vifaa tiba vya kujikinga na magonjwa ya milipuko  kwa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa Hospitali ya Rufaa Morogoro.

“Kufuatia mvua hizi, ni wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara damu, na yale yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue, endapo wananchi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema ” Amesema Gallet.

Gallet, amesema kufuatia kujitokeza kwa uharibifu wa miundo mbinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka hali hiyo ina hatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko.

Aidha, Bi.Gallet , amewakumbusha wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa kuchemsha maji kabla ya kunywa au kuyatibu kwa dawa maalumu na kuhakikisha maji ya kunywa na yale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi.

“Tunawapongeza wananchi na kuwaomba pia wanahabari kwa kuendelea kutoa elimu katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu kwa sababu wananchi wamekuwa wasikivu na kutii masharti ya usafi na jinsi ya kujikinga" Ameongeza Gallet.

Hata hivyo,amewaasa mama na Baba lishe kupika vyakula kwenye mazingira safi na kuhakikisha vyombo visafi na vyakula vinakuwa namoto kwa ajili ya kulinda afya ya mteja.

Mwisho, Gallet,  amesisitiza kutumia ipasavyo vyoo na hasa kipindi hiki cha mvua kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara hasa, kabla ya kula, baada ya kula na baada ya kutoka chooni...

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.