RC MALIMA AZITAKA HALMASHAURI KUWA NA MIKAKATI YA KUONGEZA VIWANGO VYA UFAULU KWA WANAFUNZI.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro ,Mhe. Adam Malima, amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kuhakikisha zinajipanga kimkakati ili kuongeza ufaulu kwenye Elimu na kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri Kitaifa kutoka mahali ulipo sasa, kwenda kwenye nafasi ya tarakimu moja(single digit) yaani nafasi ya kwanza hadi ya tisa.
Kauli hiyo ameitoa Januari 04/2024 akiwa katika ziara ya kukagua miundombinu ya elimu pamoja na Shule mpya zilizojengwa kupitia mradi wa BOOST pamoja na ujenzi wa madarasa mapya Manispaa ya Morogoro.
RC Malima, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ,ameshawekeza katika sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu ni jukumu sasa la Halmashauri kwa kushirikiana na waalimu pamoja na watendaji wengine wa idara ya Elimu kuongeza bidii katika maeneo yao ili waweze kuufikisha mkoa katika nafasi ya tarakimu moja (single digit) kwa kuwa sababu, uwezo na nia ya kufika hapo ipo.
“Watu wa Sekta ya elimu Ombi langu kwenu wakati tukiwa tumepata miundombinu bora ya kujifunzia pamoja na shule za kisasa , tudhamirie kuongeza bidii ili tuingia kwenye ‘single digit’, sababu za kuingia kwenye ‘single digit’ zipo, uwezo upo kwa kuwa ninyi mpo na nia ya Morogoro kuonekana juu tunayo” Amesema RC Malima.
"Katika mkoa wetu wa Morogoro tumepata shule 17 mpya kupitia mradi wa BOOST ,zaidi ya Bilioni 10 ,Rais Samia katupatia wana Morogoro, hii haijawahi kutokea tangia tupate uhuru, kilichobakia watoto wajae shule na wasome pamoja na kutengeneza matokeo makubwa ya ufaulu jambo ambalo ndio zawadi pekee kwa Rais wetu" Ameongeza RC Malima.
Aidha, RC Malima,amesema akigundua kuna watoto hawajui kusoma na kuandika ,wa kwanza kuondoka ni mwalimu kisha wazazi watafunguliwa mashtaka ,huku akisema suala la mtoto wa kike asisome limeshapita zamani watoto wote wana haki ya kusoma ili waje kuliongoza Taifa.
Pia,amewataka wazazi kushirikiana na waalimu kwa karibu ili kuongeza viwango vya ufaulu na kujua mienendo ya watoto wao na sio kuwaachia waalimu peke yao katika malezi.
Katika ziara hizo, RC Malima,ameweka majiwe ya Msingi kwa shule mpya mbili zikiwemo Shule ya Msingi Mgaza Mindu pamoja na Shule ya Msingi Viwandani Mafisa.
Mwisho,RC Malima,amewataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto wote wenye sifa ya kuandikishwa darasa la kwanza waandikishwe ili wakasome .
Post a Comment