DC NSEMWA AWATAKA WANANCHI KUENDELEA KUCHUKUA TAHADHARI MVUA ZA ELNINO.
KUFUATIA tahadhari zinazoendelea kutolewa mara kwa mara na Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA), kuhusu mvua kubwa zinazoendela kunyesha, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa ,amewataka Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari Ili kukabiliana na hali hiyo.
Hayo ameyasema kwenye Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa Januari 25/2024.
DC Nsemwa, amewataka viongozi hususani Madiwani kwa kushirikiana na Viongozi wa Mitaa kutoa Elimu Kwa Wananchi Ili waweze kujiandaa kukabiliana na mvua za elnino ambazo zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
"Ndugu zangu kama tunavyoendelea kuhimizwa na mamlaka ya hali ya hewa, mvua zinazidi kunyesha na maafa mmeona yanatokea katika maeneo yetu na mengine hadi kupoteza uhai wa wananchi wetu, kwa hiyo niendelee kusisitiza tuchukue tahadhari kwa kuweka mazingira wezeshi kwa kipindi hicho ili kujiepusha na athari zisiendelee kutokea zaidi " Amesema DC Nsemwa.
Pia amewasisitiza wananchi kila mmoja kuchukua hatua katika eneo lake ili kujilinda na maafa yanayosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema licha ya miundombinu mingi kuharibika , Manispaa tayari katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga fedha kwa ajili ya kununua Greda ambalo litatumika katika kuboresha miundombinu ya barabara kwenye Kata zake zote 29 ili kurahisisha mawasiliano ya huduma ya usafiri.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema Manispaa tayari ishachukua hatua za makusudi ikiwemo kutoa elimu juu ya wananchi wanaoishi kwenye mikondo ya maji pamoja na kuwauzia wananchi hao viwanja eneo la kiegea kwa bei nafuu ili wahame katika maeneo hayo.
Post a Comment