DC NSEMWA AWATAKA WAZAZI KUSHIRIKIANA NA WALIMU KWENYE MALEZI, ARIDHISHWA NA KASI YA USAJILI WANAFUNZI
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amewataka wazazi wa wanafunzi kuwa kiungo muhimu baina ya walimu na wanafunzi katika malezi bora na kuwasaidia wanafunzi kufaulu.
Kauli hiyo ameitoa Januari 08/2024 wakati wa ziara yake ya kukagua wanafunzi waliowasili shuleni ikiwemo usajili wa wanafunzi kidato cha kwanza na uandikishwaji wa wanafunzi wa awali na darasa la kwanza Shule za Manispaa ya Morogoro.
“Niwashukuru ninyi wazazi kwa kufika kwenu kuwasjili wanafunzi, mmeonesha ushirikiano kwa wanafunzi wetu kwa ajili ya kuwapatia elimu, ninyi ni sehemu na msaada mkubwa kwa ajili ya kuwawezesha walimu waweze kutimiza majukumu yao ya kuwalea na kuwafundisha wanafunzi wanapokuwa shuleni, na kwa wale wanaoshindwa kutimiza majukumu yao kama wazazi ndio usumbufu ambao walimu wanaupata kutokana na ushirikiano mdogo kati ya wazazi na walimu na kupelekea matokeo yasiyo mazuri kwa wanafunzi kuanzia malezi hadi taaluma, niwaombe wazazi tuendelee kutoa ushirikiano kwa walimu kwa ajili ya kumsaidia mwanafunzi kupata elimu bora na malezi bora”.
DC Nsemwa , amewataka wanafunzi wanapokuwa shuleni kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
"Wanafunzi niombe sana kufuata kanuni na taratibu za shule, na nyinyi wazazi msiwabughuzi waalimu wangu kwa kuwa wamechukua jukumu lenu la kumuadhibu mtoto katika kuwajengea malezi bora, kwa hili nitasimama na waalimu wangu,hatutamuonea aibu mtu,hatutarudisha nyuma msimamo wetu wa kisheria, tutaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaokwenda kinyume na utaratibu wa shule”Ameongeza DC Nsema.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Gabriel Paul, amesema wapo tayari kuhakikisha matokeo ya wanafunzi yanapaa juu na kuifanya manispaa kuwa kinara wa kuongoza kupata ufaulu wa kiwango cha juu ngazi ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Kaimu Divisheni ya Awali na Msingi, Stephene Mkulia, amesema matarajio ya wanafunzi kujiunga na elimu ya awali ni 7827 ,wavulana 3825 na wasichana 4002 huku upande wa wanaosajiliwa darasa la kwanza matarajio ni 10143,wavulana 5016 na wasichana 5027.
Miongoni mwa Shule ambazo DC Nsemwa ,amezitembelea ni Shule ya Sekondari Morogoro na Shule ya Msingi Mlimani Kata ya Boma.
Post a Comment