Header Ads

UWT WILAYA YA MOROGORO MJINI YAKABIDHI MSAADA WA THAMANI YA MILIONI MOJA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO MANISPAA YA MOROGORO



WAATHIRIKA  wa mafuriko , Manispaa ya Morogoro,  waliopoteza ndugu zao, makazi, pamoja na mali, wamepatiwa misaada ya kibinadamu yenye thamani ya zaidi ya Milioni Moja ( 1,000,000/=)  na Umoja wa Wazazi Wilaya ya Morogoro Mjini ambapo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Rebeca Nsemwa amepokea msaada huo akiambatana na Mkurugenzi wa Manispaa na Mratibu wa Maafa na Afisa Tarafa .

Misaada hiyo iliyotolewa Januari 29/2024,  inajumuisha  vyakula na vifaa vingine kama vile nguo , ikiwa lengo ni kutoa msaada muhimu baada ya janga hilo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Katibu wa UWT Mkoa wa Morogoro , Mwajabu Maguluko, kwa niaba ya Uongozi wa Wilaya ya Morogoro Mjini,  amesema UWT inaungana na familia za wahanga na kutoa misaada ya kibinadamu.

Maguluko ,amesema msaada huo unalenga kutoa faraja na msaada wa msingi ili kusaidia katika kurejesha hali ya kawaida kwa wahanga wa mafuriko.

'“Hali hii ya wahanga wa mafuriko imeweza kuwagusa kwa kiasi kikubwa wanawake hawa wa Morogoro, ambapo kwa pamoja wameweza kusaidia vitu hivi vyenye thamani ya shilingi Milioni Moja ( 1,000,000/=)' Amesema Maguluko.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa,ameishukuru UWT kwa kutoa msaada huo huku akisema kwamba  wataugawa kwa ufasaha ili uweze kuwasaidia wahanga  wa mafuriko.

"Nawashukuru sana UWT  hakika hili ni jeshi la Mama,namshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ametengeneza jeshi imara, uwepo wenu ni sawa na kupata taswira ya Dkt. Samia, endeleeni na moyo huo huo lakini tunaomba Taasisi nyengine ziguswe na maafa haya ziige kama UWT wanavyofanya ya kuwakumbuka wenzetu walipatwa na maafa" Amesema DC Nsemwa.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, ameipongeza UWT Wilaya ya Morogoro  kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii, hasa kwa wahanga wa mafuriko katika kipindi hiki ambacho baadhi ya wakazi wamepoteza vitu na kuharibiwa miundombinu ya makazi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.