Header Ads

WAHUDUMU WA AFYA YA JAMII MANISPAA YA MOROGORO WAKUTANA KUJADILI UTEKELEZAJI AFUA ZA LISHE NA UKUSANYAJI WA TAARIFA ZA LISHE NGAZI YA JAMII


WAHUDUMU wa Afya ngazi ya Jamii Manispaa ya Morogoro  wamekutana katika kikao kazi chenye lengo la  utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe na ukusanyaj wa taarifa za lishe ngazi ya jamii.

Kikao kazi hicho kimefanyika ukumbi wa Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro Januari 18/2024.

Akifungua kikao kazi hicho, Afisa Lishe Manispaa ya Morogoro, Jackline Mashurano, amesema kuwa  jamii inapaswa kuwa na uelewa mpana kuhusu maswala ya lishe ili kupunguza na kumaliza athari za utapiamlo katika jamii.

Aidha, Mashurano,  amewataka CHW  wameendelea kuhamasishwa kuwasaidia wananchi katika maeneo yao ili watekeleze afua hizo kwakuwa mabalozi wazuri kwa jamii inayowazunguka kutambua umuhimu wa lishe bora.

"Tumeitana hapa kuelimishana namna ya ukusanyaji wa taarifa za lishe, lakini niwaombe muendelee  kuihamasisha jamii inayowazunguka kuwa na desturi  ya kula mlo kamili, kuwaelimisha  wajawazito katika maeneo yao umuhimu wa kuanza huduma ya kliniki mapema na kuwa na mahudhurio yanayoshauriwa , ikiwa ni pamoja na ushiriki wa baba  katika kuwezesha ujauzito salama na kumpunguzia mama kazi  ili kupata muda wa kupumzika kuwezesha uzazi salama “Utapiamlo hauna ushirikina ni kuzingatia Lishe bora " Amesema Mashurano.

Katika hatua nyengine, Mashurano,  amewaomba Watendaji wa Kata  kuwaalika watoa huduma ngazi ya jamii katika mikutano ya hadhara kila mara wanapokutana na wananchi ili kuweza kuendelea kuijengea jamii uelewa wa maswala ya lishe. 

Pia, Mashurano, amewashauri watendaji wa Kata  kuielimisha jamii kuweka ziada ya chakula wakati wa mavuno na sio kuuza chakula chote ili kiisaidie jamii kwani ukosefu wa lishe bora husababisha utapiamlo ambao watu wengi katika jamii hudhani kuwa ni ushirikina.

Kwa upande wa mratibu wa Chanjo Manispaa ya Morogoro, Philipo Bwisso,  amewataka watoa huduma ngazi ya jamii kuhakikisha wanaongeza kasi ya kutambua watoto ambao wamekosa chanjo .

Bwisso , amesema kwa sasa Serikali  ipo kwenye maandalizi ya kampeni kubwa ya Chanjo ya surua ambayo inatarajiwa kufanyika mwezi Aprili 2024.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.