Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAPOKEA VIFAA VYA KUJIKINGA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imepokea vifaa tiba kwa ajili ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa na  Afisa Afya Mkoa wa Morogoro, Bi. Prisca Gallet,  kwa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa Hospitali ya Rufaa Morogoro.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro , Ndimile Kilatu amesema   vifaa hivyo vitasaidia kupunguza hatari ya watoa huduma kuambukizwa wanapotekeleza majukumu yao.

“Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti magonjwa ya milipuko hususani Mkurugenzi wetu ambapo kwa kushirikiana na timu ya Menejimenti imejipanga kikamilifu  kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa Wananchi juu ya kujikinga na Magonjwa yatokanayo na milipuko; sambamba na kuhakikisha tahadhari zote muhimu zinachukuliwa” Amesema Kilatu.

"Nitoe rai kwa wataalam wa afya kwa ngazi ya jamii, kuendelea kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko kwa wananchi ili mwananchi aweze kujikinga na magonjwa hayo, pia mama lishe na baba lishe wahakikishe kuwa vyakula vinakuwa sehemu salama na vinakuwa vya moto wakati wote " Ameongeza Kilatu.

Vifaa hivyo vya kujikinga na magonjwa ya mlipuko vimetokana na msaada wa Shirika la Afya Duniani (WHO ) kwa kushirikiana na UNICEF.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.