DC NSEMWA ATAKA TAHADHARI DHIDI YA MAGONJWA YA MLIPUKO.
MKUU wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Rebeca Nsemwa, amewataka wananchi wa Wilaya ya Morogoro kuchukua tahadhari za makusudi kujikinga na magonjwa ya mlipuko ukiwepo ugonjwa wa kipindupindu ambao tayari umefika katika baadhi ya mikoa.
DC Nsemwa, ametoa tahadhari hiyo Januari 23/2024 , wakati akizungumza na wafanyabiashara , Mama na Baba lishe Stendi ya Mabasi Msamvu akiambatana na timu ya wataalamu wa Manispaa ,Uongozi wa Manispaa akiwemo Mstahiki Meya Mhe. Pascal Kihanga na Mkurugenzi wa Manispaa, Ally Machela.
Aidha, DC Nsemwa, amesema ugonjwa huo upo japo kwa Morogoro bado haujafika hivyo kuna kila sababu ya wananchi kuchukua tahadhari ili kujilinda na magonjwa hayo ya mlipuko.
"Mpaka sasa katika wilaya yetu hatujapokea wagonjwa wa kipindupindu, lakini baadhi ya mikoa ugonjwa huo upo, niombe sana tuwe wasafi wa kila kitu kinachotuzunguka katika mazingira yetu, afya ndio msingi wa kila kitu ,kama hatutakuwa na afya nzuri hata hizi kazi zetu hatutaweza kuzifanya vizuri,tuzingatie usafi tuepuke magonjwa haya ya mlipuko" Amesema DC Nsemwa.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wananchi kuendelea kuelimishana juu ya kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya Mlipuko.
"Tumeona mvua nyingi zinaendelea kunyesha, mvua kama hizi huja na magonjwa ya mlipuko ,niwaombe wananchi wachukue hatua stahiki za kuzingatia kanuni za afya pindi mnapotumia maji muangalie pia usalama wa maji ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuhara " Amesema Kihanga.
Kwa upande wa Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu, amesema timu yake ya afya ipo kamili na wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko pamoja na kunyunyiza dawa ya Chlorine katika maeneo ya vyoo ili kudhibiti bakteria na virusi pamoja na kugawa chroline kwa ajili ya kuweka usalama wa maji kwa watumiaji.
Miongoni mwa shughuli ambazo DC Nsemwa, ameziongoza Msamvu ni kutoa elimu ya usalama wa maji kwa matumizi ya binadamu kwa kutumia kiwango cha Chlorine kilichopo kwenye maji ili kudhibiti virusi na bakteria na kunyunyiza dawa ya Chlorine vyooni kwa ajili ya kuua vijidudu vya bakteria na virusi.
Post a Comment