Header Ads

WANATAALUMA YA SHERIA VYUONI WAASWA KUTUMIA TAALUMA ZAO KWA USTAWI WA TAIFA.




MWANASHERIA kutoka Ofisi ya sheria Manispaa ya Morogoro, Alson Kireri, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kwenye kikao kazi cha wanataaluma wa sheria kutoka kikundi cha Youth Led Movement, amewataka wanataaluma hao kujitoa kwa kuwasaidia wanyonge na masikini kuweza kupata haki zao na sio kutumia taaluma katika  kuwatetea watu wanaofanya uhalifu.

Kauli hiyo ameitoa Mei 18/2023 katika kikao kazi cha wanataaluma hao cha kujadili njia sahihi za kufanya kwa wanataaluma hao katika kuisaidia jamii hususani kulinda maadili ya Mtanzania kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano  Edema Hotel Msamvu. 

Kireri,amesema  kuwa kuna watu wanakosa haki kutokana na kukosa msaada wa kisheria, hivyo kama kikundi kitumie fursa hiyo kufika mitaani kuwafundisha sheria ili wananchi wajue haki zao na wajibu wao.


Amesema kama wanataaluma hao wa sheria kwa kushirikiana na wenzao katika vyuo mbalimbali  wakijitoa kwa moyo mmoja watakuwa wamesaidia wananchi kupata haki pamoja na kupunguza migogoro iliyopo.

"Wapo Vijana ambao wanatoa msaada wa kisheria kwa kushirikiana na vituo vya kisheria , hawa wanaonesha  uzalendo mkubwa naomba na nyie mkatumie taaluma yenu kuwatumikia  wananchi" Amesema Kireri.


Mwakilishi wa Wanasheria waliojitolea  kutoa msaada wa Kisheria, Georgia  Kamina amesema kuwa wamesaidia makundi mengi ikiwa ni pamoja na kukutana na wananchi.

Naye Katibu wa Vijana CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Sabrina Juma,amesema kwa kuwa yeye anabeba jukumu la kuwalea Vijana atahakikisha elimu ya sheria Vijana wake wanaifahamu na kuleta mabadiliko chanya kwa Jumuiya yake anayo iongoza.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Youth Led Movement,Asia Ashraf, amesema lengo la kikao kazi hicho walichokiandaa ni kutokana kugundua kuwa  wananchi kushindwa kujua sheria na jinsi ya kupata haki zao.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.