Header Ads

RC Malima awaaga wachezaji wa Pamba FC, awaasa kutokata tamaa

_Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliyehamishiwa akitokea Mwanza, Mhe. Adam Malima amewaaga wachezaji wa timu ya soka ya Pamba FC iliyopo ligi ya Championship na kuwataka kutokata tamaa katika michezo yao ijayo ya Mchujo kuwania kucheza ligi kuu ya NBC kwa msimu ujao._ 

_Akizungumza na wachezaji na viongozi wa timu hiyo leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Malima amesema anaamini bado Pamba ni timu bora yenye uwezo wa kucheza Ligi kuu cha msingi ni wachezaji waongeze bidii._ 

_"Sina shaka na nyie nimewaona uwezo wenu uwanjani, naamini dawati lenu la ufundi litafanya mkazo eneo la umaliziaji ili muweze kufunga mabao mengi,"amesema Mhe.Malima._ 

_Malima amewasihi kushinda mchezo ujao wa mchujo dhidi ya Mashujaa FC utakaopigwa kwenye Dimba la Lake Tanganyika Mei 21, 2023 Mkoani Kigoma ili kurahisisha kazi mpambano wa marudiano utakaorindima uwanja wa Nyamagana Mei 28 2023._ 

_Aidha, katika hafla hiyo Mkuu huyo mpya wa Mkoa wa Morogoro amewakabidhi wachezaji jumla ya Shilingi Milioni 3 ahadi yake ya fedha Shs Milioni moja pamoja na fedha kutoka kwa mdhamini wao Kampuni ya vinywaji baridi ya Jambo Shs Milioni 2._ 

_Akitoa neno la shukrani kwa moyo aliouonesha kwa kuipambania timu hiyo Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoani Mwanza MZFA,Vedasto Lufano amesema wataendelea kumkumbuka Mhe. Malima kwa vitendo kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kucheza ligi kuu ya NBC._ 

_"Hatuna namna yoyote ya kukufurahisha zaidi ya kutimiza ndoto zako ukiwa hapa Mkoani Mwanza kuiona Pamba FC ikicheza Ligi kuu ya NBC, hilo nakuahidi tunalipambania". Lufano_ 

_Nahodha wa Pamba FC, Jerryson Tegete amesema licha ya kukosa nafasi ya kufuzu moja kwa moja na badala yake wameingia mchezo wa mchujo wamejipanga kuwapa faraja wana Mwanza kuiona timu hiyo ikicheza Ligi kuu._ 

_"Mhe.Malima kwa ari uliyotupa licha ya kuhamishiwa Morogoro hii ndoto yako ya kuiona Pamba FC inacheza Ligi kuu, kwa niaba ya wenzangu tunakuahidi kuitimiza," Tegete._ 

_Pamba FC imemaliza michuano ya Ligi ya Championship msimu huu ikiwa nafasi ya tatu na mtaji wa pointi 59,hivyo kwa kanuni za TFF italazimika kucheza mchezo wa mchujo na Mashujaa FC waliomaliza wakiwa nafasi ya 4_

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.