Header Ads

WAJUMBE BMK MAFIGA WATOA POLE KWA KANISA ANGLIKANA KUFUATIA KUUNGULIWA NA NYUMBA YA WATUMISHI WAO.



WAJUMBE wa BMK Kata ya Mafiga wametoa pole kwa Kanisa Kuu la Utatu Mtakatifu Dayosisi ya Morogoro Anglikana kufuatia kuunguliwa na nyumba ya watumishi wao ambayo waliinunua kwa ajili ya ukarabati.

Wajumbe hao wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, Mei 9/2023 walitembelea nyumba hiyo ya watumishi iliyounngua.

Akizungumza katika eneo hilo la tukio na wahanga pamoja na Viongozi wa Kanisa hilo, Mhe. Butabile, ametoa pole kwa wanafamilia kuunguliwa na nyumba na vitu vya thamani  huku akisema sio muda wa kuzungumza mengi  kwa sababu kila mtu sasa yupo katika hali ya masikitiko na hata tathimini inaweza kuwa ngumu kwa sasa kufanyika lakini ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba hakuna mtu aliyepoteza maisha.

“Hizi mali zinatafutwa lakini uhai hautafutwi hivyo licha ya kupoteza kila kitu kwa kuteketezwa kwa moto hatuna budi kushukuru kwa uhai, kwahiyo niwaombe pamoja na hii changamoto basi mtulize moyo. Sasa katika hali hii wakati tukisubiri kuona nini cha kufanya nikitoka hapa nitalifikisha  Ofisi ya Kata , Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro pamoja  na Ofisi ya Mkuu wetu wa Wilaya na Ofisi ya Mbunge ili kuona ni kwa namna gani na sisi tunaweza kufanya kitu" Amesema Butabile.

“Sote tunafahamu ajali haipigi hodi hivyo katika hilo nitumie fursa hii kuwaomba pia majirani zetu wengine mwenye chochote kwa ajili ya hawa ndugu zetu basi anaweza kukiwasilisha ili tuwasaidie, kama tulivyojionea kila kitu hapa kimeteketea hivyo tuendelee kuwafariji huku tukiwaombea hawa ndugu zetu utulivu wa moyo”Ameongeza Butabile.

Naye Askofu Jimbo la Anglikana, Askofu Godfrey Sehaba, ameushukuru Uongozi wa Kata ya Mafiga chini ya Diwani Butabile kwa kuwa na moyo wa kipekee kuwakimbilia katika janga walilokumbana nalo.

"Huu ni Uongozi wa kipekee, sina cha kuwalipa lakini yote haya yametokana na sisi viongozi wa kidini kushirikiana vyema na Serikali , mmetutahmini sana, kufika kwenu ni faraja tosha kwetu kuona wapo ndugu ambao ukiwa na jambo wana kukimbilia, tuendelee kushirikiana maana hata katika Kanisa letu wapo waumini ambao ni wananchi wa Kata ya Mafiga, ushirikiano udumu na kuendelee kutoa elimu juu ya mafundisho ya kujitoa kwa wengine, pia nichukue nafasi hii kuwaombea Viongozi wetu wa Serikali ,  Rais wetu wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutimiza majukumu yake na watendaji wake" Amesema Askofu Sehaba.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.