Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAKABIDHI WATOA HUDUMA YA AFYA YA UZAZI VIBAO 29 VYA UPIMAJI VIASHIRIA VYA LISHE KWA WATOTO CHINI YA MIAKA 5 .

MANISPAA ya Morogoro imewakabidhi watoa huduma wa Kliniki ya afya ya uzazi,Baba, mama na Mtoto vibao 29 kwa ajili ya kupima viashiria vya lishe kwa Watoto chini ya miaka 5.

Vibao hivyo vimegaiwa Mei 30/2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Shabani Duru, ukumbi wa Soko Kuu la Chifu kingalu Morogoro.

Akizungumza wakati wa kufungua Mafunzo kwa watoa huduma hao, Duru, amesema ujio wa vibao hivyo utasaidia kwa kiasi kikubwa Kliniki kupima viashiria vya lishe kinachoainisha urefu/kimo na umri ( udumavu) kwa Watoto chini ya miaka 5.

Duru amesema, athari za udumavu ni nyingi ambazo hupelekea Watoto kuwa hatarini kupata magonjwa sugu Kama moyo, saratani na mengineyo.

" Udumavu unawapa mzigo mkubwa wakiwa wakubwa katika kufikiri, uwezo wa kuchambua mambo, kutafakari kwake na hata kuelewa kwake masomo darasani, Kuna wakati unaweza kumchapa na kumpa adhabu Kali Mtoto darasani ukadhani anafanya makusudi kutoelewa kile anachofundishwa , kumbe akili yake ilidumaa kwa kukosa lishe tangu utotoni" Amesema Duru.

Mwisho, amewataka watoa huduma wa afya kutoa huduma kwa uwaledi na kutunza vifaa vizuri ili kuendelea kuboresha afya, lishe na ustawi wa Wananchi wa Manispaa ya Morogoro.

Kwa upande wa Muuguzi Mkuu wa  Manispaa ya Morogoro, Reinfrida Isack, akimwakilisha mganga mkuu Manispaa,amesema Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa sehemu zenye udumavu kwa asilimia 26.4 kufuatana na tafiti za lishe kwa TNNS, 2018.

" Upatikanaji wa vibao hivyo vitasaidia kujua Watoto wenye udumavu na kuweza Kuandaa afua sahihi katika kukabiliana na udumavu na kuweza kujipima wapi tunatoka na wapi tunakwenda"  Amesema Rainfrida.

Naye Afisa lishe Manispaa ya Morogoro, Jackline  Mashurano   amesema Manispaa imekuwa na changamoto ya katika mfumo wa afya wa taarifa ( DHIS2) juu ya taarifa ya uwiano wa urefu na umri chini ya miaka 5, hivyo vibao 29 vya kuanzia vitaongeza na kuboresha utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa taarifa zitakazo anzia katika kitabu namba 7 Cha Watoto na baadae kuingizwa katika mfumo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.