Header Ads

MWENYEKITI YANGE AZINDUZA OPERESHENI SIMIKA BENDERA UVCCM WILAYA YA MOROGORO MJINI.


MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana CCM , Ndg. Mwishehe Yange, amezindua rasmi operesheni Simika bendera pamoja na ziara ya  kuimarisha uhai wa Jumuiya na Chama Wilaya ya Morogoro Mjini.

Uzinduzi huo umefanyika Mei 26/2023 katika Viwanja vya Kata ya Mazimbu kwa kupandisha bendera pamoja na zoezi la upandaji wa miti.

Akizungumza katika uzinduzi huo, CDE. Yange, amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwajenga vijana kuwa wazalendo huku akiwataka vijana kukisemea chama na Serikali na kazi zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika hatua nyengine, amewataka Vijana kutojiingiza katika makundi yasiyofaa badala yake wasimame mstari wa mbele kukisema chama na kuangalia fursa ili wasonge mbele.

Kwa upande wa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Morogoro, Ndg. Ally Simba, amesema siasa  ni maisha ya Watu Siasa ni Watu Pia, hivyo amewapongeza Vijana wa CCM kwa kubuni wazo lenye matokeo makubwa ya baadae kwa vizazi vijavyo.

Simba, amezitaka Wilaya nyengine ziige mfano wa Morogoro Mjini kwani wilaya ya Morogoro Mjini wamekuwa mstari wa mbele wa kutekeleza maagizo ya Viongozi haraka mara wanapopata taarifa.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Morogoro Mjini, CDE Kudra Mdeng’o, amesema  lengo la kusimika bendera ni kuwaonesha watu Jumuiya haijalala ipo kazini pamoja na kuimarisha uhai wa Jumuiya.

“Tunaamini idadi kubwa ya wapiga kura  ni vijana na sisi ni viongozi wa vijana tuna jukumu kubwa la kuwafikia vijana popote pale walipo maana kutokana na shughuli zao za kiuchumi ni vigumu kukutana nao kwa pamoja sehemu moja hivyo tumeamua kuwafuata huko huko site walipo ili tuzungumze nao Vijana wenzetu” Amesema Mdeng’o.

 

Pamoja na ziara hiyo ya kuimarisha uhai wa Jumuiya, amesema lengo lengine ni kukutana na Vijana wa Bodaboda katika vituo vyao na kuzungumza nao juu ya mambo makubwa anayofanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mwisho, Mdeng’o, amewaomba  wananchi na viongozi wengine kuendelea kumuunga mkono Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Dkt. Abdulaziz Abood, kwa jitihada zake za kuhamasisha  miradi ya maendeleo na kusimamia kikamilifu fedha zinazotolewa na Serikali katika ujenzi  wa miradi ya maendeleo.

Katibu wa Vijana CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Sabreena Juma,amewaonya na  kupiga marufuku vijana kuwa Chawa kwa lengo la kutafuta uongozi au kipato na kuwataka kutumia njia sahihi za kupambania Chama kwa kuwa kina utaratibu mzuri wa kuwapika na kuwapata viongozi sahihi.

“Vijana lazima tuonyane,Chama chetu kina utaratibu mzuri wa kuoka na kuandaa upatikanaji wa viongozi sio kujipendekeza na kuwa machawa ila vijana wenzangu kazi zetu ndizo zitakazotupambanua na kutuweka mahali panapostahili”Amesema Sabreena.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.