KIPIRA AWATAKA WAZAZI KUSIMAMIA MALEZI YA WATOTO WAO.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Salum Kipira, amewasihi wazazi na walezi kuwa, licha ya kubanwa na shughuli za kujiingizia kipato, pia wanao wajibu wa kusimamia malezi ya watoto wao.
Ametoa wito huo kwa njia ya simu Mei 15/2023 ikiwa Dunia ina adhimisha Siku ya familia duniani ambapo Mkoa wa Morogoro maadhimisho hayo yamefanyika Manispaa ya Morogoro Uwanja wa mpira Shule ya Msingi Mwere.
Kipira ,amesema kuwa wito huo ameutoa kutokana na vitendo vya ubakaji na ulawiti kushamiri katika jamii.
Amesema matukio ya ulawiti yamezidi kuongezeka katika jamii, huku takwimu zikionesha wanaofanya vitendo hivyo wengi wao ni ndugu wa karibu, hivyo amewahimiza wazazi na walezi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao, ili kuisaidia jamii kukomesha vitendo hivyo na kuwabaini wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Sisi kwa upande wa Jumuiya yetu ya wazazi masuala mazima ya malezi yanatugusa, siku kama ya leo nimeona nitumie fursa hii kutoa wito kwa wazazi lakini pia kuwataka Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ngazi ya Kata na Matawi kuhakikisha wanaandaa semina na kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa jinsia" Amesema Kipira.
Post a Comment