DIWANI wa Kata ya Lukobe, Mhe. Selestine Mbilinyi, amewataka Vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM Kata ya Lukobe kuwa wazalendo , kudumisha umoja pamoja na kufanya kazi kwa bidii.
Kauli hiyo ameitoa, Mei 06/2023 akiwa mgeni rasmi wakati akizungumza katika Kikao cha Baraza la Vijana wa Chama hicho katika Ukumbi wa Iswilo Manyuki Mwisho.
Akizungumza na Baraza hilo, Mhe. Mbilinyi, amesema kuwa Chama cha ASP, wakati kinaanzisha kiliona umuhimu wa kuwaunganisha vijana kwa kuweka utaratibu maalum wa kuwaandaa vijana kuwa na uzalendo wa kuipenda nchi yao na kuweza kuwa warithi wa taifa hili hapo baadae.
Mbilinyi, amesema kuwa kazi ya Wanachama ni kukisaidia Chama na Sio chama kuwasaidia wanachama , hivyo amewataka Vijana kuthamini jitihada za Chama cha CCM, na kuwa na uzalendo wa kuipenda nchi yao.
Hata hivyo, amewaomba Viongozi wa Chama wa Kata ambao ndio walezi wa Jumuiya ya Vijana kuhakikisha inawaandaa Vijana katika malezi mazuri kwani bila kuwaandaa vijana Kata inaweza ikayumba kwani wanahitaji kuona wanaandaliwa kiakili, elimu, kinidhamu, kimaadili na kupewa mafunzo yatayoweza kuwajengea uzalendo.
Katika kuona Vijana wanapatiwa Semina katika kujua mipaka ya kiutendaji wao, ameahidi kuchangia shilingi 100,000/= kwa ajili ya kuwezesha kufanyika kwa semina hiyo ambayo Uongozi wa Kata wa Chama utasimamia.
"Nafurahishwa na utendaji wenu wa kazi, mtambue kuwa Chama cha CCM, kimeona umuhimu wa kuwaunganisha vijana na ndio maana kimeamua kuwaundia Umoja wa Vijana , kutokana na hali hiyo, ipo haja sasa ya kujenga umoja iliu ili tuweze kufanya kazi kwa ushirikiano na kuufanya umoja wetu kuwa tegemeo kwa vijana wengine" Amesema Mbilinyi.
" Changamoto haziishi, changamoto zinapunguzwa twendeni mitaani tutembee vifua mbele kuwa Chama Serikali vinatimiza wajibu wake, kwa muda mfupi Kata yetu ya Lukobe tumeweza kujenga madaraja 3, lakini hata Mitaa isiyo na umeme tumeweka umeme, tumejenga Kituo kikubwa Cha Polisi cha Kata , tumejenga madarasa 9 na Ofisi moja kupitia nguvu za Wananchi na tunaenda Kuanzisha Tena madarasa 2 kwa kuwa Lukobe tuna Wananchi wengi Sana, Ujenzi wa Shule ya Sekondari Lukobe pamoja na Kituo cha afya, haya yote ni Maendeleo makubwa na yote yametokana na nguvu za Wenyeviti wetu wa Mitaa tuwasemehe vizuri., tuna kila sababu ya kukiamini Chama , Viongozi wetu bila kumsahau Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025" Ameongeza Mbilinyi.
Kuhusu suala la Ofisi,amesema Chama kina eneo na tayari katika eneo hilo ameshamwaga Kokoto na Mchanga na kwa kuanzia atajenga Msingi wa Jengo hilo kwa fedha zake binafsi na sehehemu iliyobakia Chama waone namna ya kumuunga mkono.
Katika kuona changamoto ya Vijana ya kuchapa taarifa zao na masuala mazima ya Steshenari, ametoa nafasi kwa kazi zote zinazo husu vijana watatumia Steshenari yake ya Shule ya Patricia kufanya shughuli zao hizo bila malipo.
Hakuacha nyuma suala zima la uhai wa Chama kwani ameahidi kutoa kadi 200 kwa Umoja wa Vijana ambapo kadi 100 za Vijana na kadi 100 za Chama ili Vijana hao waingie katika Mfumo wa uanachama.
Mwisho, Mhe. Mbilinyi ametumia nafasi hiyo ya kuwashukuru Vijana kupata nafasi za Uongozi 2022 pamoja na kushiriki vema kwenye uchaguzi Mkuu wa 202o na kuhakikisha Chama hicho kinapata ushindi Mkubwa, ambapo amewataka wajipange na uchaguyzi wa 2024/2025 kwa umoja wao katika kutetea maslahi ya Chama Cha Mapinduzi.
Naye Katibu Hamasa UVCCM Wilaya ya Morogoro, Jumanne Hussein, amempongeza Diwani wa kata hiyo kwa kufanya kazi kubwa ya kuiletea Lukobe Maendeleo.
"Nimpongeze Diwani wetu kwa kushirikiana na Diwani wa Viti Maalum, Viongozi wa Chama, Wenyeviti wa Mitaa, Mabalozi pamoja na Jumuiya ya Vijana, bila kumsahau Mbunge wetu Dkt. Abdulaziz Abood kwa kuhakikisha wananchi wa Morogoro Mjini hususani wa Kata ya Lukobe wanapata huduma bora" Amesema Jumanne.
Jumanne, amewataka Vijana kuwa wazalendo, kusoma kanuni na Katiba ya CCM pamoja na Miongozo yake ili kujiimarisha kisiasa na kiutendaji.
Mwisho, amewataka Vijana kuendelea kumuombea Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kumsemea kwa kazi kubwa anazofanya za kuiletea Maendeleo Watanzania.
Upande wa Kaimu Katibu wa Vijana Lukobe, Miriam Mwinyimvua, ameushukuru Uongozi wa Kata chini ya Diwani Mhe. Mbilinyi, Diwani wa Viti Maalum Mhe. Aisha Kitime ,Viongozi wa Chama wa Kata wa Chama , Viongozi wa Kata wa Serikali , Viongozi wa Serikali za Mitaa, Jumuiya za Chama na Vijana kwa kufanikisha Baraza hilo hukua kiahidi kuendelea kutoa ushirikiano yeye na Vijana wake katika shughuli za Chama na Serikali.
Post a Comment