Header Ads

DC NSEMWA AZINDUA MRADI WA KISIMA SHULE YA SEKONDARI TUBUYU WENYE THAMANI YA MILIONI 18.2 CHINI YA USIMAMIZI WA EGG TANZANIA NA USHIRIKIANO WA HOPE FOR KIDS YA USWISI

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amezindua mradi wa kisima wenye thamani ya Shilingi Milioni 18.2 mradi uliofadhiliwa na Shirika la Hope for Kids la nchini Uswisi na kusimamiwa na Shirika la Education Gauge for growth Tanzania (EGG) lenye makao yake makuu Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza katika uzinduzi huo, DC Nsemwa, ameutaka Uongozi wa shule kuhakikisha kutunza miradi ya maji na kuwa walinzi wazuri wa miundombinu hiyo ambayo wadau wamekuwa wakisaidia kwa ajili ya wanafunzi kupata huduma bora ya maji.

"Niwashukuru EGG Tanzania, kwa kushirikiana na Hope for Kids kutoka Uswisi,  mradi huu utawasaidia sana  wanafunzi wa shule hii ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiteseka na suala la upatikanaji maji,naomba mshirikiane  kwa pamoja katika kuhakikisha kwamba kuna uwajibikaji katika matumizi sahihi ya maji na kuhifadhi mazingira "  Amesema DC Nsemwa.

DC Nsemwa, amezipongeza baadhi ya shule mbalimbali ambazo zimekuwa mstari wa mbele kutunza huduma ya miradi ya  maji ikiwemo shule ya sekondari Sumaye, Tushikamane, Nanenane  kwa usafi na utunzaji bora wa miundombinu ya miradi hiyo ya maji.

Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro na Afisa Elimu Sekondari, Gabriel Paulo, amesema Manispaa ya Morogoro itaendelea kutambua  michango ya wadau wa maendeleo huku akitoa pongezi kubwa kwa EGG Tanzania na washirika wake Hope for Kids kwa kusaidia shule za Manispaa uchimbaji wa Visima.

"Nawashukuru sana EGG Tanzania jambo ni kubwa mmelifanya, niombe nina visima 15 katika shule zangu za Sekondari na nina uhaba wa visima 14 , ikiwapendeza katika miradi yenu inayoendelea niombe mnipatie visma vyengine maana bado taaasisi zetu za elimu maji ni changamoto" Amesema Gabriel.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa EGG Tanzania, Jumanne Mpinga, ameishukuru Serikali kwa kutoa fursa kwa asasi za kiraia kushiriki moja kwa moja katika kusaidiana na Serikali kwenye utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi ikiwemo elimu ambayo ndio msingi mkuu wa maendeleo ya jamii yoyote ile.

"Mkuu wa Wilaya mradi huu umefanikiwa kupitia jitihada za pamoja kati ya Serikali yetu, washirika wa maendeleo wa Hope for Kids kutoka nchi ya Uswisi, na wananchi wa Morogoro kwa ujumla, tunaamini kuwa miradi hii itakuwa na athari kubwa katika maisha ya wanafunzi wetu na jamii yote kwa ujumla" Amesema Mpinga.

Mpinga, amesema EGG Tanzania linaendesha mradi wa  "maji safi na salama shuleni"  (School Clean and safe water project ) nchini ambapo mradi huo umegawanyika katika sehemu tatu ikiwemo miradi midogo ya pampu za kusukuma kwa mkono au ( hand pump project ), miradi ya saizi ya kati ambayo miradi yake huwekwa miundombinu ya mnara na tanki la maji ambapo unabeba koki zisizo pungua 9 hadi 10 za kutoa maji huwekwa katika kuta za mnara kama mradi wa maji Tubuyu pamoja na miradi mikubwa  ambayo inahusisha kuchimba na kujenga miundombinu ya usamabazaji wa maji katika kila kitongoji cha kijiji au Mitaa.

Aidha , ameishukuru timu ya wataalamu waliofanya utafiti. timu ya wahandisi wa EGG Tanzania waliosimamia uchimbaji na ujenzi, na timu nzima ya wafanyakazi wa EGG Tanzania ,Bodi ya Shule , wazazi ,  Mkuu wa shule ya sekondari Tubuyu, waalimu  na wanafunzi kwa ujumla waliojitolea katika namna mbalimbali kuona mradi huo unafanikiwa.

Mwenyekiti wa Wazazi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Ndg. Salum Kipira,ameipongeza Asasi ya  EGG Tanzania na kusema kuwa  wamekuwa msaada mkubwa hususani katika kutatua changamoto za kijamii haswa katika utekelezaji wa miradi ya maji shuleni.

Naye Diwani wa Kata ya Tungi, Mhe. Namala Mchunguzi, ameishukuru EGG Tanzania,kwa kuwakumbuka wanafunzi wa shule hiyo ambao walikuwa hawana huduma hiyo ya maji muda mrefu jambo amablo lilikuwa likipelekea  kutembea umbali wa muda mrefu kutafuta maji na wengine kuwa watoro wanapopata nafasi ya kutoka nje ya shule.

Mwakilishi wa Diwani Kata ya Boma na Mtendaji wa Kata hiyo, Prisca Mawala,ameishukuru EGG Tanzania kwa msaada huo wa kisima huku akiushukuru Uongozi wa Tungi chini ya Diwani wake kwa kuilea vyema shule hiyo licha ya shule hiyo kuwa chini ya Kata ya Boma.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.