Header Ads

RC SHIGELA AWAPONGEZA MANISPAA YA MOROGORO KWA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO.












MKUU  wa Mkoa wa Morogoro, Mhe.  Martine Shigela, amewapongeza Viongozi na watendaji wa Manispaa ya Morogoro  kwa Mshikamano mzuri katika utekelezaji wa Miradi ya Kimaendeleo.

Kauli hiyo ameitoa , Mei 18/2022  wakati wa Ziara yake ya Kikazi ya Kukagua Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro  ikiwemo kukagua matumizi bora ya fedha za Mapato ya ndani na zile za Serikali Kuu za Miradi Mbalimbali ya maendeleo.


RC Shigela,  amebainisha kuwa amefarijika kuona utekelezaji wa maagizo ya kamati ya Bunge ya kila Halmashauri yenye mapato makubwa kujenga kituo kimoja cha Afya na madarasa kadhaa ili kuinua Shule za msingi unaendelea vizuri ikiwemo ukamilishaji wa miradi hiyo katika kata za Tungi na Lukobe katika Manispaa hiyo.


“Kwa hiyo mimi nimefurahi kuona kwamba Maagizo ya Kamati sasa tunajenga kituo cha Afya tayari milioni 250 zimekwishaletwa hapa kupitia mapato yenu ya ndani, nawapongeza kwa hilo” Amesema RC Shigela.

“Lakini nimefarijika zaidi kuona kwamba katika Mapato yenu ya ndani nje ya kujenga Kituo kimoja cha Afya mmekamilisha ujenzi wa Zahanati sita na Madarasa 53 ambapo kati ya hayo yalitokana na mapato ya ndani ni 45, hayo ndio mambo ninayotaka kuyaona katika Manispaa hii” Ameongeza RC Shigela.

Katika hatu nyingine, RC Shigela, amemuelekeza Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Msimamizi wa mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Lukobe kinachojengwa kutokana na fedha za tozo Tsh. 1.2Bil. kumsimamia vema Mkandarasi wa Ujenzi huo ili kukamilisha ujenzi huo kabla au ifikapo June 30 Mwaka huu 2022.

Kwa upande wake, Mstahiki  Meya wa Manispaa ya Morogoro,  Mhe. Paschal Kihanga, amebainisha kuwa Miradi ya Elimu na Afya iliyokamilika na inayoenda kukamilika inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi kulingana na kada husika hivyo, amemuomba Mkuu wa Mkoa kushughulikia changamoto hiyo ili wananchi waweze kuhudumiwa kikamilifu.

Naye Diwani wa Kata ya Lukobe Mhe. Celestine Mbilinyi ,ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za ujenzi wa Kituo hicho ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi wa eneo hilo.

Hadi sasa kiasi cha Shilingi milioni 250 zimekwishapelekwa kituoni hapo kwa ajili ya kuharakisha ujenzi huo wa kituo nhicho ambacho umefikia asilimia 75% ya kazi hiyio.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.