Header Ads

TAS MOROGORO YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA VYAMA VYENGINE VYA WALEMAVU

Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Morogoro, Hassan Mikazi, akizungumza katika mdahalo wa ajira Jumuishi.
Afisa Ustawi Manispaa ya Morogoro, Rehema Malimi, akizungumza katika mdahalo wa ajira Jumuishi.

Viongozi wa TAS, Afisa Ustawi Manispaa , na Viongozi wa Asasi za watu wenye ulamavu wakiwa katika picha ya pamoja.

CHAMA Cha watu wenye Ualbino Mkoa wa Morogoro (TAS), kimeahidi kuendeleza ushirikiano baina ya vyama vyengine vya Walemavu.

Kauli hiyo ameitoa  Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Morogoro, Hassan Mikazi , katika mdahalo na Asasi za watu wenye ulemavu juu ya ajira Jumuishi iliyofanyika Ofisi Kuu ya TAS iliyopo Kata ya Kilakala Manispaa ya Morogoro April 30/2022.

Akizungumza na Waandishi wa habari , Mikazi, amesema TAS,itahakikisha inatoa ushirikiano wa dhati kwa Asasi zenye watu wenye ulemavu kwani kufanya hivyo kutaimarisha umoja wao na kuweza kupiga hatua.

Mikazi, amesema , kwa sasa mikakakti yao ni kuona watu wenye ualbino wanapewa vipaumbele kama ilivyo watu wengine ili kuweza kuweka na kujenga usawa .

Aidha, amesema mdahalo huo ni wapili kufanyika kwani katika mdahalo wa kwanza walishirikisha Waandishi wa habari ili kuweza kufikisha ujumbe kwa haraka juu ya ajira jumuishi.

Kuhusu suala la mkopo wa asilimia 2 ya watu wenye Ulemavu,  Mikazi amesema, ni vyema Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na maafisa ustawi wa jamii wakahakikisha wanawasaidia watu wenye ulemavu wanapokabiliana na changamoto kwenye uandikaji wa maandiko ya kuomba mikopo.

“Unakuta kikundi cha watu wenye ulemavu wanakuwa wabunifu na wanawazo zuri la kuanzisha mradi au biashara lakini wanakumbana na changamoto ya kuaandaa andiko la miradi yao na hivyo kuwafanya wakate tamaa mapema,” Ameongeza Mikazi.

Mwisho, Mikazi amepongeza Ustawi wa Jamii Ngazi ya Mkoa na Manispaa kwa jitihada ambazo wamekuwa wakizifanya katika kutetea Watu wenye Ulemavu.

Naye Afisa Ustawi Manispaa ya Morogoro , Rehema Malimi, amevitaka vyama vyote vya watu wenye ulemavu kuwa kitu  kimoja ili waweze kufikia malengo. 

Malimi, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua na kutekeleza jukumu lake la kuhamasisha na kuwalinda watu wenye ulemavu nchini kwa kuhakikisha haki za kundi hilo maalumu zinatekelezwa.

“Tunafanya  kazi kwa ushirikiano mzuri na Vyama vya Watu wenye Ulemavu ikiwamo  kuangalia namna bora ya kuwahudumia kwa kuzingatia mahitaji yao, niombe tu vyama wawe na umoja na washikamane ili zile fursa zinazotokea waweze kuzipata kwa umoja wao , kikubwa walemavu waendelee kushirikiana kikamilifu na kushikana mikono wanapopata fursa " Amesema Malimi.

Malimi, amesisitizia umakini wa kuwachagua viongozi katika kipindi cha chaguzi zao ili Viongozi watakao wachagua wawe wenye ualedi wa kuwatumikia na kuleta mabadiliko.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Salumu Ally, amesema bado asilimia 3 ya waajiri kuajiri watu wenye ulemavu ni changamoto na kuiomba Serikali kuangalia upya suala hilo.

Pia Salumu , amewataka Walemavu na Vyama vyao kuwa na ushirikiano jambo ambalo litawafanya kuonekana na kupiga hatua kama ilivyo vyama vyengine.

Mradi wa ajira jumuishi ni mradi wa miezi 3, yaani kuanzia mwezi 4/3-5/6 /2022 ambapo umekuwa ukiendeshwa kwa njia ya midahalo kupitia kutoa elimu ya kuhamasisha makundi ya rika, jinsi na hali zote kuwathamini watu wenye ulemavu na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali ambapo mdahalo wa kwanza ulianza na  Waandishi wa habari, ukafuatiwa na Asasi za watu wenye ulemavu ambao ndio walengwa na unatarajia kukamilisha  kwa  waajiri wa Taasisi mbalimbali zikiwemo binafsi na Serikali.

Katika Mdahalo huo, Asasi za watu wenye ulemavu  walikubaliana kuweka mikakati ya pamoja ya kufanya  ikiwamo kujenga uwezo vikundi vya watu wenye ulemavu kupitia mradi wa pamoja (kujitambua, kuhamasisha , kupata usajili , kupata fursa mbalimbali na namna ya kuzifikia, kushirikisha waandishi wa habari kupata taarifa ambapo  TAS wamejitolea kuhakikisha mpango huo unafanyika , kuwajengea uwezo wazazi namna ya kuwalea watoto kama watoto wa kawaida wasiokuwa na ulemavu-malezi jumuishi, walezi na vijana shuleni kuwa na malezi jumuishi, kuhusisha viongozi wa dini na wadau mbalimbali juu ya ajira jumuishi (advocacy -elimu ya kutambua ajira jumuishi, kujengea uwezo watu wenye ulemavu kisheria na kikanuni na kujiamini (kuweza kusimamia sheria), Asasi za watu wenye ulemavu ziwe na kanzi data zenye taarifa za watu wenye ulemavu kuweza kupata taarifa ambapo fursa zinapatikana iwe rahisi kutumia data na hata taarifa zifanane kwa taasisi na Serikali, Kuibua vipaji na kuwajengea uwezo walemavu waweze kujiajiri (kuandaa bonanza la watu wenye ulamavu kwa Mkoa wa Morogoro, Kuendeleza ushirikiano kuanzia kwenye jamii wanazoishi na asasi za watu wenye ulemavu. 


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.