Header Ads

MUHIMBILI YAZINDUA MRADI WA KLINIKI WA KUSAIDIA WAGONJWA WA SELIMUNDU NA HAEMOPHILIA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA MOROGORO.

Maandamano kuelekea eneo la tukio.

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) ikishirikiana na wadau wa afya Novo Nordisk Haemophilia Foundation (NNHF) , Novo Nordisk foundation (NNF) na Kenya Haemophilia association (KHA),Mei 20/2022  imezindua  mradi wa ujenzi wa Kliniki ya Selimundu na Haemophilia ambao utasaidia upatikanaji wa haraka na ukaribu wa huduma , vipimo na matibabu kwa wagonjwa wa Haemophilia na Selimundu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa Muhimbili, Dkt. Stella Rwezaura amesema kwa mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Kenya.

“Lengo kuu la mradi huu  ni kuwezesha upatikanaji wa vipimo vya magonjwa haya katika hospitali zote za rufaa nchini , upatikanaji wa wataalamu wa afya waliobobea kwenye magonjwa haya pamoja na upatikanaji wa miundombinu sahihi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hawa,” Amesema Dkt. Rwezaura.

Dkt. Rwezaura, amesema kuwa mradi utasaidia uanzishwaji wa Klinic  za Haemophilia na Selimundu kwenye hospitali zote za rufaa  pamoja na kutoa mafunzo elekezi kutoka kwa wataalamu wabobeza wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, utaziwezesha hospitali za rufaa kuanzisha na kutoa huduma za mazoezi tiba kwa wagonjwa (Physiotherapy) Pamoja na vipimo maalumu vya kugundua magonjwa haya mapema.

Amesema kuwa  asilimia 97 ya wagonjwa wa haemophilia hawajui kama wanaougonjwa huo na hawajawahi kupatiwa vipimo vyovyote ili kujua hali ya ugonjwa, hivyo wengi hujikuta wakihusisha ugonjwa huo na ushirikina.

Aidha, amesema kuwa ugonjwa wa Selimundu tayari umeshafanyiwa tafiti mbalimbali ambazo zimesaidia uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa  na kuwezesha kuwepo kwa mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa na pia umewekwa kwenye mpango mkakati wa kitaifa wa magonjwa yasiyoambukiza.

“ Hata hivyo, amesema  Tanzania inasadikika  kuwa na wagonjwa wa haemophilia kati ya 6000 hadi 12000 nchini, lakini wanaofahamika na wanaoendelea na matibabu 167 tu.“Mradi huu utasaidia kuongeza kasi katika upatikanaji wa takwimu za ugonjwa wa Hemophilia , utasidia kufanyika tafiti za ugonjwa huu na pia utaharakisha uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa hawa pamoja na kuweka ugonjwa wa Hemophilia katika Mpango mkakati wa magonjwa yasiyoambukiza (NDC) na hatimaye kuwa na mwongozo wa utoaji huduma (National Treatment Guadline ) kwa ugonjwa huu katika Hospitali zote nchini” Ameongeza Dkt. Rwezaura.

Naye, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dkt. Daniel Mkungu, ameishukuru Hospitali ya Muhimbili kwa kuanzisha mradi huo wa Kliniki ya wagonjwa wa Selimundu na Haemophilia katika Hosdpitali hiyo huku akisema kuwa Haemophilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda ambao unasababishwa  ukosefu wa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu na  kusababisha damu kuvuja kwa muda mrefu.

Dkt. Mkungu, amewataka  wananchi kufika hospitali ya Rufaa katika Kliniki hiyo  mara moja pale wanapokuwa na viashiria vya kutokwa damu mfululizo kwa muda mrefu unapotokea mchubuko, kukatwa au kujikata.

Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 123,113,716/= ikiambatanisha gharama za vitendanishi vya Maabara , Vifaa vya physiotherapy na dawa.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.