MEYA KIHANGA AWATAKA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA CHA WATOTO WAKIWA SHULENI.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga, (kushoto) akimkabidhi zawadi mwanafunzi aliyefanya vizuri katika masomo .
MSTAHIKI wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wazazi kuwa na desturi ya kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao mashuleni ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwani watoto wengi wamekuwa wakifeli kutokana na utoro.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa hafla iliyoandaliwa na Uongozi wa Shule ya Msingi Mazimbu 'A' ya kuwasilisha taarifa ya shule hiyo kwa wazazi wa wanafunzi hao iliyofanyika leo Juni 3/2021 katika viwanja vya shule hiyo.
Mhe. Kihanga, amesema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikizikabili shule nyingi ni kutokana na wazazi kutochangia fedha kwa ajili ya chakula cha mchana kwa watoto wao hali ambayo huchangia kuwepo kwa utoro kwa watoto ambao hawali mashuleni.
Amesema kuwa kutokana na baadhi ya wazazi wengi kutokuwa na mwamko wa kuchangia chakula mashuleni, kumekuwa kukichangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwepo kwa division kwa upande wa shule za Sekondari lakini ufaulu usioridhisha kwa wanafunzi , hivyo amewaomba wazazi husuani wa shule za Msingi na Sekondari kuweza kutoa ushirikiano wa kutosha kwa ajili ya elimu ya watoto wao kwa kuchangia fedha kwa ajili ya chakula ili watoto waweze kusoma kwa utulivu."Kwa kweli uwepo wa baadhi ya wazazi wengi kutochangia chakula cha mchana kwa ajili ya watoto wao ndio wamekuwa wakichangia shule zetu kuweza kupata matokeo yasiyoridhisha, kwani wengi wa wanafunzi wanaopata ziro na wale ambao hawali chakula cha mchana hapa shuleni, hivyo tunawaomba sana wazazi wachangie chakula cha watoto ili tuhakikishe tunafuta division ziro."Amesema Mhe. Kihanga .
Katika hatua nyengine, amechukua nafasi ya kuwapongeza Waalimu wa Shule za Msingi Mazimbu A na B kwa kufanikiwa kufaulisha wanafunzi kwa kila mwaka hususani katika upande wa shule za Serikali Manispaa ya Morogoro.
Aidha, amesema licha ya changamoto walizozitaja , atahakikisha kwa kushirikiana na Uongozi wa Shule zote 2, pamoja na wananchi wanaendeleza desturi ya kujenga darasa moja kwa kila mwaka ili kuondokana na changamoto za mrundikano wa wanafunzi katika darasa moja.
Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazimbu A, Mwl. Anitha Nathan,amesema kuwa kuna mambo mengi yanayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu katika Shule zao za Msingi ikiwemo Wanafunzi kutokupata chakula cha mchana mashuleni hali inayowafanya watoto kutofuatilia masomo ipasavyo.
"Tumepokea wito kutoka kwa Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Morogoro , kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa la kuwataka wazazi kuchangia cha mchana cha Wanafunzi, upande wetu tumeshawaita wazazi waweze kuchangia , lakini bado katika upande huu hatujaweza kuanikiwa sana , niwaombe sana wazazi waendelee kuchangia kwani tukichangia michango hii ya chakula itakuwa ni jambo ambalo litasaidia sana watoto wetu kuweza kusoma kwa umakini wakiwa wameshiba na wakaelewa vipindi darasani wakiwa wameshiba"Amesema Mwl. Nathan.
Aidha, amesema licha ya changamoto ya chakula lakini zipo changamooto mbalimbali ikiwemo changamoto za uhaba wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi wa kike na wakiume, mshahara kwa ajili ya mlinzi n.k.
Mbali na hafla hiyo ya wasilisho ya taarifa kwa wazazi juu ya mienendo ya shule hiyo ikiwamo changamoto , mafanikio pamoja na nini kifanyike, lakini wameendesha zoezi la kuwatunukia zawadi wanfunzi waliofanya vizuri katika masomo tofautitofauti na kutambua vipaji vyao.
Mwisho, Mstahiki Meya , ameendesha zoezi la harambee la wazazi kuweza kuchangia walichonacho ili kuweza kuwatia moyo waalimu wanaopambana na wanafunzi shuleni katika kuhakikisha wanaongeza ufaulu kwa wanafunzi hao na kuinua viwango vya elimu ambapo mwisho wa harambee hiyo jumla ya shilingi 80,000/= ilipatikana kupitia michango ya wazazi walioguswa na harambee hiyo .
Post a Comment