JUMUIYA YA WAISLAMU AHMADIYA WAENDESHA MKUTANO MKUBWA KAHAMA, WAHAMASISHA AMANI.
Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislam Ahmadiyya Tanzania Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, akizungumza kwenye mkutano wa dini na wanajumuiya hiyo katika Msikiti wa Wigehe Manispaa ya Kahama.
Na Marco Maduhu, Kahama
Jumuiya ya Waislam Ahmadiyya, imeendesha mkutano mkubwa wa kidini wa mwaka katika viwanja vya msikiti wa Ahmadiyya uliopo Wigehe Manispaa ya Kahama.
Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na viongozi wa Jamaati, na Masheikh wa jumuiya hiyo ya Ahmadiyya kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, na kuongozwa na Amir na Mbashiri Mkuu wa Ahmadiyya Tanzania Shekh Tahir Mahmood Chaudhry.
Sheikh Chaudhry akizungumzia lengo la mkutano huo, amesema dhumuni lake kubwa ni kutoa mafundisho ya kidini kwa wana jumuiya, pamoja na kuwafanya wawe raia wema wenye kuishi kwa upendo na kudumisha amani ya nchi.
Amesema Jumuiya hiyo ya Waislam Ahmadiyya, imekuwa ikiendesha mikutano mikubwa kila mwaka hapa nchini, ili kuwafanya wanajumuiya hiyo kuishi kwenye miongozo ya kidini.
"Jumuiya yetu ya Waislam Ahmadiyya tunaata wana jumuiya wawe watu wema, na siyo kuwa watenda maovu wala kujihusisha kwenye masuala ya ugaidi na migomo, sababu dini yetu hairuhusu kufanya fujo bali ni kuishi kwa amani,"amesema Sheikh Chaudhry.
Pia amesema Jumuiya hiyo inapinga sana vitendo vya baadhi ya wananchi kuendekeza masuala ya imani potofu za kishirikina, hasa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, na kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, wazee na wenye Ualbino.
Katika hatua nyingine Chaudhry amesema, mbali na jumuiya hiyo kutoa mafundisho ya kidini na hata kujenga Misikiti 21 mkoani Shinyanga, pia wamekuwa wakichangia huduma za kijamii ambapo wamejenga visima vya maji 150 mkoani humo, ili kuwaondolea wananchi changamoto ya ukosefu wa maji salama.
Kwa upande wake Sheikh wa Jumuiya ya waislam Ahmadiyya kutoka mkoani Mbeya Karim Shams, aliwataka wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema, pamoja na kufuata misingi ya kidini.
Nao baadhi ya wanajumuiya hiyo ya Ahmadiyya waliohudhuria mkutano huo wa kidini, walisema mafundisho hayo yamekuwa msaada mkubwa sana katika imani zao.
Post a Comment