MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA MKOA WA MOROGORO ZATAKIWA KUTENGA BAJETI KWA AJILI YA HUDUMA ZA USTAWI .
MAMLAKA za Serikali za Mitaa zimetakiwa kutenga bajeti kwa ajili ya utoaji elimu na usimamizi wa huduma za ustawi wa Jamii.
Hayo yalisemwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro Bi. Jesca Kagunila wakati wa kikao kazi cha siku moja cha kuwajengea uwezo mafisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri zote za Mkoa huo kilichoandaliwa na Mkoa kwa kushirikiana na Mdau wa Mradi wa Kizazi kipya Kanda ya Kati kupitia Shirika la PACT TANZANIA
Akizungumza katika kikao kazi hicho Afisa Ustawi wa Jamii Jesca alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakapotenga bajeti ya kutosha Mamlaka rahisi kusimamia masuala ya Ustawi ya Jamii bila kuwepo changamoto zozote katika sehemu zao za kazi na kuwawezesha kutoa huduma kwa weledi na ufanisi.
Jesca alisema Maafisa Ustawi wa Jamii wamekuwa wakishughulika na Jamii hivyo watakapotengewa bajeti ya kutosha itasaidia kuifikia jamii kwa ukubwa na wakati.
"Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa kuhakikisha vikao vya mabaraza ya Wazee ,Watu Wenye Ulemavu na Kamati za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinafanya kila robo kama ilivyoainishwa kwenye sera, sheria na miongozo" alisema Jesca .
Aidha aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha takwimu za watoto ,wazee na watu wenye ulemavu zinahuishwa na utambuzi unafanyika kwa kuwashirikisha Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na kujadiliwa kwenye vikao vya vijiji, kata na halmashauri.
Pia wawe na ratiba ya utoaji wa vipindi kwenye vyombo vya habari sambamba na utoaji elimu mashuleni na vyuoni.
Akizungumzia suala la mimba/ndoa za utotoni na Ukatili wa Kijinsia amesisitiza umuhimu wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Halmashauri/Wilaya
kujadili masuala hayo na kuweka mikakati ya namna ya kuondoa au kupunguza matukio hayo kwenye Jamii.
Alisema kwamba masuala ya ukatili kwa watoto, mimba/ndoa za utotoni ni suala mtambuka si la kuwaachia Maafisa Ustawi wa Jamii pekee, kwa kuwa Maafisa wa kada hiyo ni wachache ukilinganisha na matukio hayo yanayojitokeza kila kukicha hivyo nguvu za pamoja zinahitajika.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi, kuwahimiza Maafisa Ustawi wa Jamii kuwapatia takwimu za matukio hayo ili ziweze kujadiliwa katika vikao vya WDC, CMT, CHMT na Kamati za Ulinzi na Usalama ili kuweka mpango mkakati wa kupunguza matukio hayo kwenye jamii" alisema Jesca.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Kusirye Ukio amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kufanya kazi kwa juhudi na maarifa huku wakijijengea tabia ya kutathmini kazi zao kwa mujibu wa maelekezo yanayotolewa na serikali sambamba na kuwahimiza Waganga Wakuu wa wilaya kufanya ufuatiliaji wa fedha zilizotengwa kutumika kwa wakati kwa ajili ya kutekeleza majukumu yaliyo chini ya kada hiyo.
Naye Meneja wa Mradi wa Kizazi kipya Kanda ya Kati Shirika la PACT Merina Shaidi alisema lengo la mradi huo ni kutoa huduma kwa watoto waliothiriwa na walioathirika na Virus Vya Ukimwi – VVU, kutoa huduma za Afya, Elimu, lishe, uchumi, ulinzi na usalama kwa mtoto.
Meneja wa Shirika hilo . Merina amewataka Maafisa ustawi wa Jamii wakati wanapoelekea mwisho wa mradia huo kuendeleza kazi ambazo zimekuwa zikitekelezwa na mradi huo ili kuhakikisha taarifa za ustawi zilizopo kwenye kata zinahifadhiwa kwa usiri mkubwa ili ziweze kutumika wakati zitakapohitajika kama mwongozo wa Serikali unavyoelekeza.
Post a Comment