ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA MOROGORO ,BW. BAKARI MSULWA, ATOA NENO HILI KWA WATUMISHI
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Bw. Bakari Msulwa, akisoma taarifa ya shukrani wakati wa makabidhiano ya Ofisi.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Bw. Bakari Msulwa, amewataka watumishi ,viongozi wa Serikali,viongozi wa vyama vya Siasa, wakuu wa idara , na vitengo kumpa ushirikiano Mkuu wa Wilaya wa sasa ili aweze kutimiza majukumu yake katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Hayo ameyasema leo Juni 22/2021 katika hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi na Mkuu wa Wilaya wa sasa Mhe. Albert Msando kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
"Napenda kumshukuru Mungu kwa muda wote nilioaminiwa na Serikali kuwa madarakani kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Morogoro , lakini nawashukuru sana viongozi wote wa Serikali kwa kunipa ushirikiano wa kutosha katika majukumu yangu, niwaombe viongozi wote wa Serikali, Taasisi mbalimbali, viongozi wa vyama vya siasa , wakuu wa idara na vitengo pamoja na wananchi wote wa Wilaya ya Morogoro tumpe ushirikiano wa dhati Mkuu wetu wa Wilaya kama mlivyofanya kwangu, kwani ushirikiano wenu ni chachu ya maendeleo kwa Wilaya yetu, " Amesema Bw. Msulwa.
Msulwa, amesema kuwaushirikiano aliyopewa akiwatumikia wananchi wa Morogoro ndio uliompa nguvu ya kuweza kuitumikia Serikali na Taifa kwa Ujumla .
Katika hatua nyengine, Bw. Msulwa, amemtoa hofu Mkuu wa Wilaya Mhe. Albert Msando, kuwa hali ya usalama wa Wilaya ya Morogoro ipo shwari na wananchi wapo tulivu wakiendelea kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo yao huku akisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ya kuzidi kuimarisha hali ya usalama kwa wananchi pamoja na mali zao.
Mwisho, Msulwa, amechukua nafasi ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweza kumuamini katika kipindi chote alichokaa madarakani huku akimtakia majukumu mema ya kujenga Taifa.
Post a Comment