WAZIRI MCHENGERWA ATOA AGIZO TAKUKURU KUZICHUNGUZA HALMASHAURI ZILIZOPATA HATI CHAFU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa ametoa agizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hapa nchini kupita kwenye kila Halmashauri zote ambazo zimepata hati chafu kwa mujibu wa Mkaguzi na mdhibiti wa hesabuza Serikali na kufanya uchunguzi.
Mchengerwa alitoa agizo hilo April 26, katika Wilaya ya Rufiji alipokuwa kwenye ziara ya siku moja kuongea na watumishi wa Halmashauri ya Kibiti na Rufiji.
Alisema kuna haja ya Halmashauri hizo kufanyiwa uchunguzi ili kubaini watendaji wasiowaaminifu na hatua za kisheria zichukuliwe.
Alisema Halmashauri hizo zinatakiwa kufanyiwa uchunguzi ili ibainike sababu ya kupata hati chafu na waliohusika ili kuondoa watu ambao si waaminifu kwenye Utumishi.
" Takukuru kwenye maeneo ambayo Halmashauri zimepata hati chafu wafanye uchunguzi ili taarifa hizo zisaidie kuona sehemu ambazo hawakufanya vizuri na kama Kuna uzembe hatua zichukuliwe" alisema Mchengerwa
Mchengerwa pia aliwataka watendaji wa TAKUKURU kuhakikisha wanahudhuria kwenye mikutano inayoitishwa na wakuu wa Wilaya kwenye maeneo yao ili watoe elimu kwa wananchi.
Aidha Waziri huyo aliwataka viongozi wa Taasisi za Umma kushughulikia mashauri ya watumishi waliosimamishwa kazi waweze kupata haki zao kisheria.
Alisisitiza pia utolewaji wa mafunzo na semina kwa watumishi zitakazosaidia kuwajenga kuendelea kuwapa waadilifu kwenye Utumishi wao.
" Viongozi wa Taasisi, wakiwemo wakurugenzi tumieni ubunifu wenu kuwapatia mafunzo watumishi, zipo Taasisi ziko tayari kusaidia kutoa semina na mafunzo, wapeni fursa watumishi hii inasaidia kukumbushana masuala ya maadili kazini tisizibe fursa" alisema.
Mchengerwa alisema Serikali ya awamu ya sita imejipanga pia kuondoa kero za watumishi ambapo wanaostahili watapandishwa madaraja na kulipwa stahiki zao.
Post a Comment