DIWANI MWEMBESONGO ATAKA SUALA LA USAFI LIPEWE KIPAUMBELE
Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana akishiriki zoezi la usafi na wananchi.
Mtendaji wa Kata ya Mwembesongo, Amina Saidi ,akishiriki zoezi la usafi na wananchi.Wananchi wakifanya usafi wa kufyeka nyasi pembezoni mwa Mfereji.
Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana pamoja na Mtendaji wa Kata , Amina Saidi, wakitoa shukrani kwa wananchi mara baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Juma Hamsini, Chande Ramadhani,akizungumza na wananchi waliojitokeza katika zoezi la usafi.
DIWANI wa Kata ya Mwembesongo Manispaa ya Morogoro, Mhe. Ally Kalungwana, ametoa mwito kwa wananchi wa Kata ya Mwembesongo , kuufanya usafi wa mazingira kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku ili kuepuka magonjwa ya milipuko, ikiwemo kipindupindu na kuhara.
Aidha, amesema maisha bora yatakuwa ndoto ya mchana endapo wananchi wenyewe hawatajitoa kuhakikisha wanauthamini usafi wa mazingira yao hasa kwa kujenga vyoo bora na kuvitunza, kusafisha maeneo yote yanayowazunguka na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni angalau kwa vipindi vitano kwa siku.
Kalungwana ,ameyasema hayo leo Aprili 24/2021, wakati wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi wa usafi ambapo usafi huo ulifanywa katika Mfereji wa Anti Malaria kwa kuwajumuisha wananchi wa Mitaa iliyo jirani na mfereji huo kwa kufyeka nyasi pembezoni mwa mto.
Amesema kuwa, endapo wananchi wataendelea kutupa taka hovyo huku huduma ya usafi katika Kata ya Mwembesongo ikiendelea kuwa duni, hakuna mafanikio yatakayofikiwa katika vita dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
“Ni wajibu wa kila mmoja kushiriki usafi binafsi na wa mazingira yanayo mzunguka ikiwemo vyoo, kuhakikisha hayawi chanzo cha maradhi ya kuhara na kipindupindu, pia suala la kunawa mikono nalo ni la muhimu na linapaswa kupewa kipaumbele zaidi, hata kama wananchi watajitoa ipasavyo kushiriki usafi wa vyoo na mazingira mengine yanayowazunguka" Amesema Kalungwana.
Aidha, Mtendaji wa Kata ya Mwembesongo, Amina Saidi, amesema kuwa usafi huo utakuwa endelevu hivyo amewaomba wananchi waweze kutoa ushirikiano ili kuifanya Kata ya Mwembesongo kuwa safi na salama.
"Yapo maeneo mengi yenye shida lakini tulikubaliana kwamba tuanze eneo hili la kimkakati kwanza kisha tutazunguka maeneo mengine yote, wito wangu wananchi wafanye usafi na suala la usafi liwe endelevu " Amesema Amina.
Amina, amesema kuwa kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi itakuwa siku ya usafi na jumamosi nyengine ni kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwili kwa kukutana pamoja na wananchi na kuanza kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zao.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Juma Hamsini, Chande Ramadhani, amempongeza Diwani wa Kata ya Mwembesongo kwa kushiriki pamoja na wananchi kufanya usafi.
Pia amesema kwa niaba ya Viongozi wenzake watahakikisha wanamuunga mkono Mtendaji mpya ili kuhakikisha mipango yote inayotakiwa kufanywa ndani ya Kata ya Mwembesongo inafanikiwa kwa iwango kikubwa.
Kwa upande wa mwananchi wa Kata ya Mwembesongo, Consolata Mtiga, ameushukuru Uongozi wa Kata chini ya Diwani pamoja Watendaji wote huku akisema kwamba watahakikisha wananchi wanawaunga mkono viongozi kwa mipango yote ndani ya Kata yao.
" Zoezi ni zuri, haya maeoeneo yalikuwa yanajificha vibaka na wezi sasa tutapata amani sana vichaka vimetolewa tutaishi kwa amani kubwa sana , kikubwa wananchi wenzangu tusiwaangushe viongozi wetu tushirikiane nao" Amesema Consolata.
Post a Comment