TBF KUENDESHA MAFUNZO YA MAKOCHA WA KIKAPU KATIKA NGAZI MBALIMBALI
SHIRIKISHO la mpira wa kikapu Tanzania (TBF) kupitia Kamisheni yake ya Makocha kwa kushirikiana na Chama cha Makocha wa Kikapu Tanzania (TBCA) wameendesha mafunzo ya Makocha wa Kikapu katika ngazi mbalimbali.
Kozi ya kwanza ilikuwa ni "Mafunzo ya makocha wa mpira wa kikapu kwa waalimu wa Shule za sekondari" Utambulisho" yaani "Introduction to Basketball" na kozi ya pili ilikuwa ni Mafunzo ya makocha wa mpira wa kikapu Daraja la kwanza Taifa yaani "Basketball Coaches course - National level 1".
Mafunzo hayo yamehitimishwa leo katika viwanja vya JMK Youth Park na Don Bosco, Upanga, Dar es Salaam.
Mgeni rasmi aliyehudhuria mahafali ya kozi ya kitaifa Don Bosco, Upanga alikuwa ni Rais wa Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF) Ndg. Phares Magesa ambaye aliwapongeza washiriki na amewataka Makocha hao wapya wakayatumie mafunzo hayo kwa vitendo kwa kufundisha timu za vijana mitaani , shule za msingi, sekondari, vyuoni na vilabu mbalimbali nchini na pia kujiandaa na awamu nyingine za mafunzo kama National level 2, FIBA level 1, 2 na 3 ili kujiendeleza zaidi.
Kozi hiyo ya kitaifa wamehitimu walimu wa kikapu 25 kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Rais wa TBF amesema mafunzo kama haya yataendelea mikoa mbalimbali nchini na yatakayofuata yatafanyika Babati, Manyara kuanzia 23 hadi 30,Aprili, 2021.
Pia amesema Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania litaendelea na mipango ya kuendeleza mchezo wa kikapu nchini kwa kutafuta wafadhili zaidi kugharamia uendeshaji wa ligi mbalimbali, program za maendeleo ya Kikapu, kuhamisha ujenzi wa viwanja vya Kikapu nchi nzima na kuendesha mafunzo ya mbalimbali ili kuinua mchezo wa kikapu kiufundi katika fani za ualimu, uamuzi, utunza takwimu, tiba za michezo na utawala katika ngazi mbalimbali za awali, kitaifa na kimataifa.
Imetolewa na:
Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF).
01.04.2021
Post a Comment