Header Ads

DIWANI MAFIGA AWATAKA BODABODA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MKOPO KUBORESHA MAISHA YAO


               

Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile akizungumza na Vijana wa Bodaboda , (kushoto) Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mafiga, Nesphora Kinoge, (katikati), Afisa Mtendaji Kata ya Mafiga, Ibrahimu Salumu Kobi.


Vijana wa Bodaboda wakimsikiliza kwa Makini Diwani wa Kata ya Mafiga.

DIWANI wa Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro , Mhe. Thomas Butabile,  amewaagiza madereva wa boda boda Kata ya Mafiga  kuanzisha na kusajili vikundi vya ujasiriamali, ili kujijengea mazingira mazuri kupata mikopo ili kuweza kuboresha maisha yao.

Kauli hiyo ,ameitoa Aprili  09/2021 katika Ukumbiwa Rose Garden uliopo Kata ya Mafiga wakati wa mkutano wa kuzungumza na Madereva wa Bodaboda wa Kata hiyo.

Aizungumza na Waandishi wa habari, Mhe. Butabile,  amewataka Bodaboda wa Kata ya Mafiga  kuchangamkia mikopo inayotolewa na manispaa  ya Morogoro  kwani mikopo hiyo haina riba na ni kwa ajili yao.

“Kwa hiyo nyinyi madereva wa bodaboda, Serikali imesogeza fursa za mkopo kwenu na Manispaa ya Morogoro  tayari imekuwa ikitenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo, mikopo hii ni kwa ajili ya kuboresha maisha yenu, msilale changamkeni, jiungeni kwenye vikundi vilivyosajiliwa muweze kupata mikopo itakayokuza mitaji yenu kwani mtambue kuwa  dereva mmoja mmoja ni ngumu mno kupata mkopo kwenye taasisi za kifedha, kwahiyo mkiwa na vikundi kama Afisa Maendeleo wa Kata alivyosema mtaweza kukukopesheka kwa makundi” Amesema Mhe. Butabile.

Akisisitiza kuhusiana na uchukuaji wa mikopo kwa malengo na urejeshaji ,Mhe. Butabile,  amesema  “ Sisi kazi yetu ni kusimamia ukusanyaji wa mapato,fedha zipatikane, ninyi kazi yenu ni kukopa, fedha zipo kwa ajili yenu,njooni mkope ,hii ni fursa ya kutoka kimaisha kikubwa kukumbuka  kwamba wanapokopa wanatakiwa  kurejesha kwani wasipo rejesha  wanapokuja wakaguzi wanakuta mikopo hairejeshwi kama inavyotakiwa ni kuitia doa na kuichafua  manispaa.

Hata hivyo amewataka, Bodaboda wote ifikapo tarehe 16 /2021 kwamba Siku hiyo ni tarehe maalumu ya kufanya uchaguzi wa kupata Uongozi wa Bodaboda wa Kata ambapo utakuwa na malaka ya kusimamia bodaboda katika Vijiwe vilivyopo Kata hiyo.

"Tunakwenda kufanya uchaguzi, nawashukuru sana Bodaboda mliofika leo japo sio wote, lakini kuna Vijiwe vingi sana katika Kata hii, niombe tunapoitwa tuwe wepesi kufika na kuitia wito, katika uchaguzi Kijiwe ambacho hakitafika tutakifuta katika Kata yetu na kukiondoa kabisa, tutengeneze nidhamu katika kazi zetu ambazo zinatuingizia kipato" Ameongeza Mhe. Butabile.

Katika hatua nyengine, Butabile, ameendelea kuwaomba wadau wa maendeleo kuendelea kutoa misaada ya hali na mali katika kuboresha miundombinu ya Elimu kwalengo la kutatua changamoto zinazoikabili sekta muhimu ya Elimu Kata ya Mafiga ikiwemo ujenzi wa Madarasa pamoja na Vyoo.

Kwa upande wa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi , Kata ya Mafiga, Farida Rajabu, amesema kuwa Serikali imeweka sheria kwa kila Halmashauri kutenga asilimia kumi (asilimia nne kwa wanawake,asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa walemavu) kutokana na mapato ya ndani na kuwapa mikopo isiyo na riba ili kuwawezesha kuanzisha miradi na kujikwamua kiuchumi hivyo ni wajibu wa vIjana hao kuanza kuchangamkia fursa hiyo.

Pamoja na kuwataka Vijana hao wa Bodaboda  kujiunga kwenye vikundi na kwenda Halmashauri kuomba mikopo hiyo vilevile lakini  amesema zipo  changamoto mbalimbali za zinazojitokeza kwenye mikopo hiyo ikiwemo ya wananchi kudhani kuwa mikopo hiyo ni misaada na hivyo hawapaswi kurejesha na baadhi ya wanavikundi kukimbia ili wasilipe mikopo hiyo.

Naye Afisa Maendeleo Kata ya Mafiga, Nesphora Kinoge, amewataka Vijana wa bodaboda kuchukua hatua ya kuunda vikundi vya ujasiriamali  ili kuweza kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri. 

Aidha, amesema kuwa  Ofisi ya Mkurugenzi  kwa kusimamia hilo imekuwa ikiendelea kusajili na kupokea miradi ya Vikundi mbalimbali ili kuweza kuvisaidia kufanikisha na kujikwamua kiuchumi .

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.