DC MSULWA AWATAKA MADIWANI MANISPAA YA MOROGORO KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO
MKUU wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Bakari Msulwa, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo ili kuwezesha Halmashauri kuweza kuongeza uwezo wa kujitegemea kwa mapato ya ndani ya halmashauri.
Kauli hiyo ameitoa leo Aprili 29/2021 katika Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro katika ukumbi wa mikutano wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mhe. Msulwa, amewataka pia Waheshimiwa Madiwani kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda vidogo, kati na vikubwa na kubuni vyanzo vyengine vya kimkakati kwani kufanya hivyo kutaongeza Mapato ya halmashauri na serikali kuu.
DC Msulwa, amewaeleza madiwani kuhakikisha kwamba wanaongeza juhudi kubwa katika kufikiria zaidi masuala ya uwekezaji na kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema halmashauri ikiboresha mapato itasaidia halmashauri kutoa huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo afya, elimu, Maji nk na pia kiwango cha mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake itaongezeka.
Hata hivyo,Mhe. Msulwa, amesema kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani lazima uendane na nidhamu ya matumizi ya fedha kwa hiyo ni jukumu la Baraza la Madiwani kusimamia na kuhakikisha kuwa mapato yote yanayokusanywa katika vyanzo vya ndani yanatumika ipasavyo.
"Ufuatiliaji wa mara kwa mara ufanyike ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa na lazima Waheshimiwa Madiwani utaratibu wa kukagua miradi hiyo inayotekelezwa na Halmashauri kupitia kamati zake ufanyike na kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo kikamilifu ili endelee kuwasaidia wananchi" Amesema DC msulwa.
“Serikali kweli inachukua baadhi ya vyanzo vya mapato lakini mrejesho wake unaonekana mfano tumepata fedha za ujenzi wa Soko Kuu , Stendi ya Kisasa, na miradi mingine ambayo tunarajia iweze kupandisha hadhi ya Manispaa yetu kuwa Jiji , hivyo sioni kama kunatatizo, tunachopaswa ni kufikiri namna ya kupata vyanzo vipya vya mapato tutakavyoweza vimudu. Ameongeza DC Msulwa.”
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mazimbu, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wataalamu kuongeza bidii kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kuisadia Manispaa kuweza kujiendesha na kufikisha huduma kwa jamii.
Naye , Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sabasaba, Mhe. Mohamed Lukwale, ameshauri waheshimiwa madiwani kusimama kwenye nafasi zao ili kuwapa nguvu watendaji katika kufanikisha lengo la kuinua mapato ya Manispaa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma, amewataka Madiwani hao kuwa na umoja na mshikamano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowasilishwa kwao kutoka kwa wananchi ili kuweza kuzitatua na kuzijadili kwa pamoja.
"Tufanye kazi kwa pamoja ,mimi siko upande wa mtu yeyote, bali nahusiana na watu wote kikubwa ni kuendelea kushrikiana na kuleta maendeleo ya Manispaa yetu ya Morogoro na kama kuna makundi tuyavunje ,CCM ni moja na tupo kwa ajili ya kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo kama tulivyo ahidi kwa wananchi" Amesema Fikiri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kwamba yeye pamoja na wataalamu wake watapambana kuanisha na kuandika maandiko mbalimbali ya maeneo ya uwekezaji ikiwa pamoja na kutafuta wafadhili watakaowezesha kufadhili na kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali na kusema kuwa ushirikiano baina ya watendaji na Waheshimiwa Madiwani unahitajika kwasababu nia ni moja ya kunyanyua mapato.
Post a Comment