HAYATI JOHN POMBE MAGUFULI ALIONESHA NJIA KWA WATANZANIA: NABII JOSHUA
Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Ararm Mwantyala, akizungumza wakati wa ibada maalumu ya kumuombea Hayati Magufuli.
Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Ararm Mwantyala , amesema Hayati Dkt John Pombe Magufuli , alionesha njia kwa Watanzania katika kuhakikisha Tanzania inapaa kiuchumi huku akipingana na vikwazo mbalimbali kutoka Mataifa ya nje ambayo yamekuwa hayaitakii mema nchi ya Tanzania.
Kauli hiyo ameitoa Machi 31/2021 katika ibada maalumu iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro ya kumuombe Hayati John Pombe Magufuli iliyofanyika katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Jamhuri.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Nabii Joshua, amesema Hayati Magufuli, alijinyima sana na kukubali kufarakana na Mataifa yanayopinga Maendeleo ya Watanzania huku kila akifanyacho alikuwa akimtanguliza Mwenyezi Mungu mbele kitu ambacho kilikuwa ndio tabia yake ambayo Watanzania tulikuwa tukiiona .
Nabii Joshua, amesema kuwa Hayati Magufuli,alipambana na rushwa , kutetea wanyonge, pamoja na miradi mingi aliyoianzisha anaamini kwamba Rais wa sasa Mama Samia Suluhu akichukua mkondo huo wa kumtanguliza Mwnyezi Mungu mbele Taifa hili litapiga hatua na kusonga mbele sana.
"Nikweli watanzania wanalia sana na hata kama mtu halii basi moyoni mwake ana hudhuni, hata Bwana Yesu wapo watu walio mlilia lakini aliwapa faraja na kuwaambia msinililie mimi angalieni maisha yenu " Amesema Nabii Joshua.
Aidha,Nabii Joshua, amesema Hayati Magufuli alikuwa Jembe la Nguvu, Serikali yake, ikajizatiti kutoa elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na kufuta michango iliyokuwa inawanyanyasa watoto wa wakulima, kwani alitambua kwamba, kwa njia ya elimu makini, hata watoto wa watanzania maskini wataweza kutoboa na hatimaye kupata maisha bora zaidi jambo ambalo linatokana na ukweli kwamba, elimu ni ufunguo wa maisha.
Amesema Katika uongozi wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Hayati Magufuli , Serikali ya Tanzania iliweza kujenga Zahanati 1, 198, Vituo vya Afya 497 na Hospitali za Wilaya ni 71. Dkt Magufuli alitambua kwamba, afya bora kwa watanzania ni mtaji katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu.
Mwisho, amewataka Watanzania kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Maisha ya Hayati Magufuli na kuwataka wayashangilie maisha yake kwani kazi aliyoifanya kwa kipindi cha miaka 5 ni kazi ambayo inapaswa kuienzi kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi hiyo kwani inawezekana kuwa Mungu alimchukua kwa kuweza kufanya alama yake isifutike .
alexandarina
Post a Comment