MKURUGENZI MANISPAA MOROGORO ATAKA JAMII KUPINGA UKATILI WA AINA ZOTE ILI KUFIKIA MALENGO YA KUWA NA KIZAZI CHENYE USAWA .
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, imeitaka jamii kuhakikisha inapinga ukatili wa aina zote ili kufikia malengo ya kuwa na kizazi chenye usawa kati ya wanawake na wanaume.
Kauli hiyo ameitoa leo Machi 08/2021, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambapo Manispaa ya Morogoro inaadhimisha siku hiyo kwa kuangazi masuala yanayowahusu wanawake katika maeno mbalimbali.
Akizungumza kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani, Lukuba, amesema kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi mwaka 2021 , kauli mbiu imelenga kutengeneza jamii yenye usawa kati ya mwanaume na mwanaume katika nafasi mbalimbali za Uongozi .
”Katika miaka ya 1990 wanawake walikuwa wanafanya kazi nyingi, ujira kidogo, unyanyasaji,hawakupewa kipaumbele ikilinganishwa na wafanyakazi wanaume, hivyo niwaase Wakina Mama wenzangu na Wanawake wote tutumie muda huu kutafakari wapi tumetoka, wapi tulipo na wapi tunakwenda ili kuweza kuwa chachu kufikia Dunia yenye usawa ” Amesema Lukuba.
Lukuba, amesema kuwa lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutathmini utekelezaji wa afua za kufikia usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, kijamii, kisiasa katika kufikia maendeleo jumuishi.
Aidha, amesema kuwa, maadhimisho hayao pia yanatoa fursa ya kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na jamii, Serikali, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi na wadau wengine katika kukuza hali ya mwanamke wakitanzania.
Pia ,amesema kuwa , katika kuadhimisha Siku hii wadau wanapata fursa ya kubainisha upungufu nambinu za utatuzi wa changamoto zilizopo.
Hata hivyo, amesema kuwa Manispaa ya Morogoro, imeendelea kutenga fedha za asilimia 10 katika mapato yake ya ndani za kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuanzisha mfuko wa uwezeshaji kiuchumi ikiwa ni pamoja na mfuko wa maendeleo ya wanawake wenye masharti nafuu ambao umesaidia kutoa mikopo nafuu na mafunzo ya stadi za biashara kwa wajasiriamali wanawake.
“Baada ya maadhimisho hayo, tutahakikisha tunatumia maadhimisho haya kwa kuandaa makongamano na majukwaa mbalimbali ili kujadili na kuibua kero zinazokwamisha maendeleo na Ustawi wa wanawake na kuyatafutia ufumbuzi ikiwemo matatizo ya maji na uchumi duni, kuangalia changamoto za Wajasiriamali wetu pamoja na kuanzisha siku maalumu ya kuwakutanisha Wajasiriamali kwa ajili ya kutangaza bidhaa zao ” Ameongeza Lukuba.
Naye Afisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe, amebainisha kilele cha maadhimisho kitakuwa na mabanda ya huduma na maonesho ya bidhaa kutoka kwa wanawake wajasiriamali na wadau mablimbali ili kuonesha kazi zinazofanywa na wanawake katikakujiletea maendeleo jumuishi.
Kadhalika, kutakuwa na shuhuda za wanawake jasiri ambao wanafanyakazi zilizodhaniwa kuwa ni za wanaume ili kuhamasisha wazazi na wasichana kufanya kazi za aina zote.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani "WANAWAKE KATIKA UONGOZI ; CHACHU KUFIKIA DUNIA YENYE USAWA
Post a Comment