MANISPAA YA MOROGORO KUKUSANYA BILIONI 11 MAPATO YA NDANI MWAKA WA FEDHA 2021/2022
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood, akipitia taarifa za Bajeti.
Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Mohamed Lukwale, akifuatilia kwa umakini Mkutano wa Bajeti.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro, Ruth John (kushoto), Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba (kulia) wakiwa katika Mkutano wa Bajeti.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 11 kupitia mapato ya ndani katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Hayo yamezungumzwa leo Machi 11, 2021, na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga, wakati wa kuwasilisha rasmi Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 katika Mkutano maalum wa Bajeti wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Morogoro katika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Kihanga, amesema Manispaa inakadiria kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi Tshs.91,002,691,864.82 ambapo kwenye mapato ya ndani ni Tshs.11,503,535,009.00 ruzuku ya mishahara na matumizi ya kawaidia Tshs.73,012,455,589.61 na miradi ya Maendeleo ni Tshs.6,506,701,265.
Kihanga, amesema mapato ya Halmashauri yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka 2019/2020 mapato ya Halmashauri yalikuwa Tshs. 6,075,926,212.87 ambapo kwa mwaka 2020/2021 ni Tshs.8,478,799,224.32 sawa na ongezeko la kiasi cha Tshs.2,402,873,011.45 sawa na asilimia 28.3.
Hata hivyo, amesema Manispaa ya Morogoro , imeendelea na utoaji wa Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kama kanuni inavyoagiza kuwa Halmashuri kupitia mapato yake ya nbdani kutenga asilimia 10.
Amesema katika bajeti ya 2020/2021 Manispaa ya Morogoro, ilitenga kiasi zaidi ya milioni 700 ambapo hadi sasa hivi zimepelekwa kiasi cha Tshs.249,963,000.0 kwa vikundi 26 ikiwa Wanawake vikundi 11 yenye thamani ya Tshs. 94,250,000.00 ,Vijana vikundi 13 vyenye thamani ya Tshs.149,713,000, na vikundi 2 vya wenye ulemavu vyenye thamani ya Tshs.6,000,000.00.
Kuhusu TASAF, amesema katika mwaka 2020/2021 jumla ya Tshs.365,318,864.00 zimetolewa kwa walengwa 2,545 katika mitaa 164 kusaidia Kaya masikini.
Kuhusu elimu, amesema ufaulu wa mitihani ya Msingi na Sekondari umeongezeka ambapo kati ya wanafunzi 8,398 waliofanya mitihani ya kumaliza Darasa la saba, wanafunzi 7,577 walifaulu sawa na asilimia 90 .
Katika Ujenzi wa madarasa ,amesema madarasa 15, matundu ya vyoo 33 na madawati 225 vilitengenezwa kupitia fedha za EP4R ambapo Manispaa ilipokea kiasi cha Tshs.336,300,000.00.
Aidha kwa upande wa sekondari, amesema Manispaa ilipokea kiasi cha Tshs.140,000,000.00 ikiwa Tshs.40,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na Tshs.100,000,000.00 kwa ajili ya ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilakala.
Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 jumla ya maabara za Sekondari 7 zilikamilishwa ambapo kiasi cha Tshs.85,000,000.00 zilitumika , miongoni mwa shule hizo ni pamoja na Kingolwira , Kayenzi, Kilakala na Sumaye.
Pia, amesema Manispaa ya Morogoro imeweza kusimamia ujenzi wa mradi wa Stendi mpya ya daladala Mafiga, Stendi ya Daladala Kaloleni, ujenzi wa Soko Kuu la Chifu Kingalu ambalo limegharimu kiasi cha Tshs. 17,655,838,405.65, ujenzi wa kitega uchumi wa DDC ambapo kwa sasa imefikia asilimia 85 ya ukamilishaji na inategemewa hadi kufikia mwezi wa nne mradi huo utakuwa umekamilika.
Katika huduma za afya, Manispaa ya Morogoro imetenga kiasi cha Tshs.300,000,000.00 kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati ya Tungi, Kihonda, Kihonda Maghorofani,Sultan Area, Kituo cha afya Sina na Zahanati ya Mazimbu.
Hali ya mipango miji, manispaa ya Morogoro imeandaa mpango kabambe wa upangaji wa mji utakaoenda mpaka mwaka 2035, hivyo Mji wa Mnaispaa unawezwa kupangwa vizuri kuendana na ongezeko la Wananchi wanaoweka makazi.
Manispaa imeendelea kujenga uwezo ikiwa ni kutoa mafunzo kwa wakuu wa idara, madiwani na wasaidizi wa wakuu wa idara ili kuweza kujua majukumu /mipaka yao ya kiutendaji , sanjari na hayo pia Mnaispaa imeweza kununua Kompyuta ,meza.viti, Scanner,A/C n.k.
Hali ya maambukizi ya UKIMWI imepungua kutoka asilimia 5.6 hadi 3.8 kwa kipindi cha Julai-Septemba, 2020 na kwa kipindi cha Oktoba -Desemba kiwango cha maambukizi kimeongezeka kwa silimia 0.5 kutoka 3.8 hadi 4.3.
Katika Mwaka wa fedha 2021/2022 Manispaa imepanga kufanya shughuli mbalimbali ambazo zimetengwa ikiwamo kuanzisha mashamba darasa 3 ya mazao ya mboga katika Kata ya Mafisa, Bigwa na Milmani, kujenga Machinjia ya kisasa yatakayogahrimu kiasi cha Tshs.180,000,000.00, ujenzi wa madarasa katika shule za Msingi ambapo kiasi cha Tshs.400,000,000.00 zimetengwa, ujenzi katika shule mbili ambazo ni Kikundi na Kiwnaja cha Ndege, umaliziaji wa Shule ya Sekondari ya ghorofa iliyopo Kata ya Boma ambapo Tshs. 400,000,000.00 zimetengwa, ujenzi wa choo cha Mtoto wa kike Shule ya Sekondari Kingo kiasi cha Tshs.40,000,000.00,umaliziaji wa maboma 4 katika Shule za Sekondari Kola, Kingolwira, Kauzeni na Bondwa kwa kiasi cha Tshs. 260,000,000.00, jumla ya kiasi cha Tshs 475,000,000.00 zimetengwa kumaliza Zahanati na Vituo vya afya vya Tungi,Sulatan Area, Mazimbu, Kiegeya, Kihonda Maghorofani , Lukobe, Uwanja wa Taifa na Mbuyuni.
Katika uwezeshaji wa kuchumi, Manispaa ya Morogoro imetenga kiasi cha Tshs. 963,000,000.00 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.
Mwisho, amewashukuru Viongozi, Madiwani , Wananchi pamoja na Waandishi wa habari kwa kuhudhuria Mkutano huo muhimu ambapo amesema pamoja na mambo mengine , bajeti hiyo imezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 -2025 na mkakati wa kukuza Uchumi na kupunguza Umasikini (MKUKUTA).
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewashukuru Wananchi wote waliohudhuria kikao maalum cha kupitisha mapendekezo ya mipango ya bajeti 2021/2022.
"Nawashukuru sana Waheshimiwa Madiwani kwa maelekezo yenu ya msingi mliyoyatoa wakati wa kujadili bajaeti hii kupitia kamati zetu za kudumu za Halmashauri, niwapiongeze Wananchi wote kupitia Mabaraza ya Maendeleo ya Kata na katika vikao vilivyofanyika katika nyakati na ngazi mbalimbali ,kwa kujitokeza kwa wingi , waandishi wa habari, napenda kuwahakikishia mawazo yenu yamezingatiwa kwa kadri ilivyowezekana katika maandalizi ya bajeti hii" Amesema Lukuba.
Katika Bajeti ya mwaka 2021/2021 , Halmashauri imelenga kutoa vipaumbele vifuatavyo, elimu , ukusanyaji mapato, usafi wa Mji, Afya, Utawala bora na miundombinu.
Post a Comment