MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO AKABIDHI LITA 145 ZA MAFUTA YA PIKIPIKI KWA MAAFISA ELIMU KATA SHULE ZA MSINGI MANISPAA YA MOROGORO.
Afisa elimu Takwimu na Vifaa shule za Msingi Manispaa ya Morogoro, Amna Kova, akisimamia zoezi la ujazaji wa mafuta ya pikipiki kwa Maafisa elimu Msingi Kata Manispaa ya Morogoro leo Machi 12/2021.
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amekabidhi lita 145 za mafuta ya Pikipiki kwa Maafisa Elimu Kata 29 wa Shule za Msingi Manispaa ya Morogoro.
Makabidhiano hayo ya mafuta kwa Maafisa elimu hao, yamefanyika leo Machi 12/2021 nje ya Sheli iliyopo jirani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro na mwakilishi wa afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro , Amna Kova, amesema kuwa hayo mafuta yatawawezesha Maafisa elimu Kata kuzungukia katika shule na kuweza kusaidia utendaji mzuri katika kuleta matokeo chanya .
"Tunamshukuru sana Mkurugenzi wetu wa Manispaa ya Morogoro, dada yangu Sheilla Lukuba, ni Mkurugenzi wetu na pia ni mama ambaye anajali sana sekta ya elimu,anatusaidia sana katika ujenzi wa madarasa lakini katika ujenzi wa miundombinu, tunamuahidi hatutamuangusha kwani tumedhamiria kuongeza ufaulu wa asilimia 100 kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba kwenda kidato cha kwanza mwaka 2022 katika mtihani watakao fanya mwaka huu 2021" Amesema Kova.
Kova, ameendelea kumshukuru sana Afisa elimu Msingi Manispaa ya Morogoro , Chausiku Masegenya, kwa uchapa kazi wake na jinsi anavyojitoa katika utendaji kazi wake wa kuhakikisha kwamba taaluma ya wanafunzi inakuwa kwa kasi kubwa na ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Kova, amewataka Maafisa Elimu Kata hao kutumia pikipiki hizo kwa lengo lililokusudiwa na Serikali katika kukuza viwango vya ufaulu kwa wanafunzi kwa kuwa Ufuatiliaji sasa utakuwa ni karibu Mno .
Amesema kuwa pikipiki hizo ambazo walikabidhiwa zitafanya kazi kubwa ya kuwawezesha maafisa Elimu kata kuwasimamia walimu katika kata zao ili waweze kutimiza jukumu lao la msingi la kuwafundisha wanafunzi kwa kuwakagua mara kwa mara Ili kujua kama wana maandalio ya masomo na mambo yote anayotakiwa kuwa nayo ili aweze kufundisha kwa kujiamini.
Aidha amesema pia pamoja na kazi nyingine nyingi lakini pikipiki hizo zinaendelea kufanya kazi ya kuwawezesha maafisa Elimu Kata kutembelea Shule na kuona utendaji kazi katika shule zao.
Naye, Afisa elimu msingi Kata ya Mindu, Frank Nyahove, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwakabidhi mafuta ya Pikipiki , huku akisema wataendelea kufanya kazi kwa bidii kwani mafuta hayo ni motisha kwao kuweza kuwa na moyo wa kujitoa zaidi ili kuleta matokeo chanya ya ufaulu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi.
Nyahove, ameishukuru idara ya elimu ya Msingi kwa kusimamia zoezi hilo kikamilifu, huku akisema kuwa Manispaa ya Morogoro lazima ing'ae katika Taaluma.
Post a Comment