Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA YA MOROGORO AWAASA WANAWAKE KUWA CHACHU YA MAENDELEO .


MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewaasa Wanawake Manispaa ya Morogoro kuwa chachu ya maendeleo kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuleta ushindani katika kuinua uchumi wa mwanamke mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Hayo ameyasema Machi 07/2021 wakati wa maandalizi  maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwenye tukio maalumu la Morogoro Women Special  Dinner katika  ukumbi wa Glonency Nanenane Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na Waandishi  wa habari, Lukuba, amesema kuwa kutokana na uwajibikaji wa wanawake ndio maana katika awamu hii ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, imeendelea kuwaamini wanawake katika nafasi mbalimbali za kiuongozi na maamuzi.

“Kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho haya inawapa nguvu wanawake kwenye kuleta maendeleo yenu binafsi, Shirika, jamii inayowazunguka na Taifa kwa jumla hasa katika kuimarisha Uchumi wa kati kuelekea uchumi wa juu, hivyo niwaombe wakina mama wenzangu tuwe na maamuzi ”, Amesema Lukuba.

“Kutokana na ufanisi na uchapaji kazi wenu kama wanawake, napenda kushirikiana na nyinyi katika shida na raha, tembeeni kifua mbele mkijua wapo wanawake wenzenu tupo katika mamlaka za maamuzi na utawala tukiendeleea kuwapambania na kuwawakilisha vyema katika kuleta maendeleo kwa jamii zinazotuzunguka." Ameongeza Lukuba.

Katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani, Lukuba, kwa kushirikiana na wanawake wa Manispaa ya Morogoro, wametoa taulo za kike kwa ajili ya kuwasaidia Wanafunzi katika shule mbalimbali katika kujistili wakati wa hedhi.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka na kwa mwaka huu Manispaa ya Morogoro imeadhimisha siku hiyo katika Ukumbi wa Morena Msamvu.

Naye mratibu wa Morogoro Women Special Dinner, Thecla Mbiki, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa anavyojitoa katika majukumu yake.

"Mkurugenzi wetu mchapa kazi, anajituma sana, kwa muda mchache aliofanya kazi hapa Manispaa yetu ya Morogoro , kuna mabadiliko makubwa, huyu ni Super Women wa kweli , tubnajivunia kuwa na mwanamke muongoza njia katika Manispaa yetu, lakini nawashukuru wakina mama Wote ambao mmejitokeza kwa wingi katika tukio letu maalumu ambalo limetuongezea heshima sisi wanawake"Amesema Mbiki.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.