‘DAYCARE CENTERS’ ZAPEWA SOMO JUU YA MALEZI SAHIHI YA WATOTO NA VITUO.
Afisa Ustawi wa Jamii ambaye pia mratibu kitengo familia na watoto Manispaa ya Morogoro, Hamisa Kagambo, akizungumza na Wamiliki wa Daycare .
VITUO vinavyojihusisha na Malezi ya Watoto maarufu kama ‘Day Care Centers’ Manispaa ya Morogoro vimetakiwa kufuata sheria na kanuni za uendeshaji wa Vituo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii ambaye pia mratibu kitengo familia na watoto Manispaa ya Morogoro, Hamisa Kagambo, katika Mkutano wa Umoja wa Wamiliki wa vituo vya malezi kutwa (Day care Centres) Manispaa ya Morogoro wa kujadili katiba yao uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kingo Soko Kuu la Chifu Kingalu.
Akizungumza
na wamiliki wa
vituo vya malezi kutwa (Day care Centres), Kagambo, amesema lengo la Mkutano
huo wa kukutana na wamiliki hao ni kujadili katiba ya Umoja huo pamoja kutatua
changamoto mbalimbali ikiwamo majengo wanayofundishia, walimu
wanaofundisha pamoja na mbinu za kufundishia ili kupata muongozo na uelewa wa
pamoja juu ya uendeshaji vituo hivyo.
Kagambo,
amesema kuwa , sio vituo vyote vinafanya vibaya lakini vipo baadhi ya vituo
ambavyo wamiliki wengi kuwa hawajui namna sahihi ya kuendesha vituo hivyo
na hawajui miongozo kuhusiana na uendeshaji wa vituo vya watoto kutwa.
“Leo tupo katika Kikao kazi na Umoja wa Wamiliki wa vituo vya
Day Care Manispaa ya Morogoro, tumeona tukutane wadau ili tujadili Katiba yetu
lakini pia tuweze kuwa na uelewa wa
pamoja kuhusu vituo vya kulea watoto kutwa na maeneo ya makazi kwa watoto
wanaoishi mazingira magumu ili sasa pale miongozo mbalimbali na serikali na
wadau wanapotaka kutoa elimu tuwe na uelewa wa pamoja na tuwe tunaelewa
nini maana ya vituo hivi” Amesema Kagambo.
“Kuwalea
watoto sio jambo rahisi, najua walezi wawatoto wanapitia katika changamoto
nyingi, nawaomba waendelee na moyo huo huo wa kuwasimamia watoto wetu , sisi
kama Kitengo cha Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro tutasimama na nyinyi na
pale mtakapo kwama Ofisi zetu zipo wazi njooni tushirikiane lango letu ni kuona
Vituo hivi vinafanya kazi nzuri na vinajiendesha kwa misingi ya sheria , kanuni
na taratibu lakini suala la usajili liwe kipaumbele kwenu “ Ameongeza Kagambo.
Aidha,
ameutaka Umoja huo mara baada ya kupata usajili, wasiishie hapo kwenye usajili
tu bali wafikirie mambo makubwa na fursa zilizopo mbele yao.
Hata
hivyo, amesema Manispaa ya Morogoro kuna jumla ya vituo vya Watoto 79 ambapo
kati ya vituo hivyo ni vituo 15 tu ambavyo vimepatiwa usajili na vituo 8 bado
vipo katika mchakato wa kupata usajili kwani tayari vilishawasilisha vielelezo
vyote.
Pia
amewaomba Wamiliki wa vituo hivyo wasiwe waoga wanapoogaizwa kuleta Taarifa zao
za kibenki ( Benk Statement) , kwani lengo la kuleta hizo taarifa ni kutaka
kujua mzunguko wa fedha katika vituo vyao.
Naye,
Afisa afya Manispaa ya Morogoro, Martin Mziwanda,amesema mkanganyiko uliokuwepo kwa wamiliki wa
vituo kushindwa kutofautisha vituo vya malezi kutwa ‘Day Care Centres’ na shule
za watoto ‘Nursery schools’, huku akipongeza muitikio mkubwa wa washiriki na
kutoa wito kwa washiriki hao kwenda kuyafanya kwa vitendo yale waliyojifunza.
Mziwanda,
amewataka wamiliki wa vituo hivyo kuzingatia suala la usafi na kuandaa maeneo
rafiki ya michezo katika vituo vyao.
Kwa
upande Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vituo hivyo, Clarence Mkwama, ameshauri vituo vingine kuanza kujumuisha watoto wenye
ulemavu na sio kuchukua watoto wasio na ulemavu pekee kwani bado kuna tatizo
kubwa la watoto wenye ulemavu kufungiwa ndani.
Mkwama, amesema kuwa
lengo la vituo hivyo ni kuandaa watoto kimalezi hivyo watoto wenye ulemavu
wanahitaji fursa hiyo pia ambapo itawasaidia sana kujitambua na kupata ujuzi wa
kimaisha ili waweze kujisaidia wenyewe kwa sasa na hata siku za usoni.
Post a Comment