Header Ads

DIWANI KALUNGWANA AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO.


Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana (kushoto) , akisalimiana na Mwanafunzi katika moja ya matukio ya ugawaji wa Madawati kwa Shule za Msingi zilizopo Kata ya Mwembesongo.

DIWANI wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana, amewataka Wananchi wa Kata ya Mwembesongo, kushiriki ipasavyo katika vikao mbalimbali vya serikali za mitaa ili kurahisisha Upangaji wa Mipango ya Maendeleo.

Mkutano huo ulifanyika Oktoba 03/2021 katika Mtaa wa Genda.

Akizungumza na Wananchi katika Mkutano wa Kata , Mhe. Kalungwana, amesema kuwa  kushiriki vema kutasaidia Kata hiyo  kupanga mipango yake shirikishi na pia jamii itatumia ipasavyo haki ya msingi kufanikisha kujenga demokrasia.

Mhe. Kalungwana, amesema kuwa changamoto kubwa kwa Wananchi ni kutoshiriki kwa asilimia kubwa katika vikao mbalimbali hali inayotoa ugumu katika utekelezaji wa maamuzi yaliyoazimiwa .

"Wananchi niwaombe sana tushiriki katika vikao lakini kubwa katika shughuli za Maendeleo, hivi karibuni tulikuwa na Kampeni ya Ujenzi wa Madarasa 15 ambapo tulianza na  Uchimbaji wa Misingi ya katika shule hizo ikiwamo Shule ya Msingi Msavu A na B, Shule za Msingi Mafisa A na B pamoja na Shule ya Msingi Mtawala, wapo waliokuwa na Moyo walijitokeza lakini wapo waliokiuka , niombe sana swala la kushirikiana ni jambo zuri sana ambalo ndio nguzo muhimu ya Maendeleo, Maendeleo yetu tutayaleta sisi wenyewe" Amesema Kalungwana.

Amesema wapo katika Mpango wa ujenzi wa Madarasa 15 kwa shule zote 5 za  Msingi huku wakikubaliana kila Mwananchi kuchangia kiasi cha Shilingi elfu 5 kwa ajili ya kukamilisha Maboma hayo ili ifikapo mwakana wanafunzi wasipate changamoto ya kusoma.

Aidha, amewataka wananchi ambao wanafanya sherehe usiku kuhakikisha wanakuwa na vibali vya kufanya shughuli hiyo huku wakizingati  muda ambao sherehe hizo  zinatakiwa kufanyika .

Naye Diwani wa Kata ya Kihonda, Mhe. Hamis Kilongo, akiwa mwalikwa katika mkutano huo , amesema Mhe. Kalungwana ni mtu wa kazi hivyo wananchi wa Kata ya Mwembesongo wana kila sababu ya kujivunia kuwa na Diwani huyo.

Kwa upande wa Diwani wa Viti Maalum Manispaa ya Morogoro, Mhe. Hadija Kibati, amesema Mhe. Kalungwana amekuwa ni kiongozi wa kujitolea na kushirikiana na wananchi.

" Tumepata Diwani mzuri, anajitoa sana, hata Mtendaji wetu wa Kata kwakweli anapambana sana, tuwape ushirikianao viongozi wetu  ili waendelee kuchapa kazi na kutuletea Maendeleo" Amesema Mhe. Kibati.

Katika Mkutano huo, Taasisi mbalimbali ziliweza kualikwa ikiwamo TANESCO, EWURA, Jeshi la Polisi, MORUWASA, Jeshi la Zima Moto pamoja na Timu ya Wataalamu wa afya kutoka Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuelimisha juu ya Chanjo ya CORONA na kutoa huduma hiyo ya Chanjo.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.