Header Ads

MBUNGE NORAH MZERU AIOMBA SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA KALI ZA KISHERIA WANAONYANYASA WATOTO

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Norah Mzeru (wapili kushoto waliosimama ) akiwa katika picha ya pamoja na Watoto wanaoishi katika Mazingira magumu, (kushoto) , Diwani wa Kata ya Mkindo, Mhe. Majuka Koira, (wapili kulia waliosimama) Mwenyekiti wa U.W.T CCM Wilaya ya Mvomero , Lidya Joseph Mbiaji.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Norah Mzeru, akionesha upendo kwa mtoto.

MBUNGE wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro , Mhe. Norah Waziri Mzeru, ameiomba  Serikali  kuwachukulia hatua kali zakisheria watu wanaowanyanyasa watoto kwa kukiuka Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.

Hayo ameyasema leo Oktoba 09/2021 katika  uwanja wa  Ofisi ya Kata ya Mkindo wakati wa kuadhimisha Siku ya  Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (U.W.T) Wilaya ya Mvomero ambapo Mhe. Mzeru alikuwa Mgeni rasmi katika Siku hiyo.

Akizungumza na Wanawake waliojitokeza katika Maadhimisho ya Siku hiyo ya Wiki ya U.W.T, Mhe. Mzeru, amesema  tathmini imebaini kuwa watoto wengi wanaojihusisha na kazi za kubeba mizigo masokoni ni matokeo ya umaskini uliokithiri kwa baadhi ya Kaya, kuondokewa na wazazi wao kwa maambukizi ya UKIMWI, migogoro ya ndoa na ukatili dhidi ya watoto.

“Huduma za ulinzi wa mtoto zinatekelezwa kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009, katika kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa Fedha 2017/18 hadi 2021/22, kwahiyo kama mpango huo umeanza kutekelezwa ni jukumu letu sasa kuona Serikali inawaadabisha vilivyo waharifu wa Watoto kwa kutoa adhabu kali ambayo watu wengine hawatarudia kuwafanyisha Watoto kazi au kufanya unyanyasaji wa kijisni dhidi ya Watoto" Amesema Mhe. Mzeru.

Aidha, Mhe. Mzeru, amesema kuwa Serikali imekuwa ikijatahidi kuwa na mikakati mbalimbali ya kukomesha  unyanyasaji ikiwemo  kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za msingi za mtoto kupata elimu na malezi bora ambapo  utoaji wa elimu msingi bila malipo umetoa fursa kwa watoto wengi wenye umri wa kwenda shule kuandikishwa kuanza elimu ya awali kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi.

"Kutoka kwenye sera ya Taifa ya watoto ya mwaka 1996 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2008 imeweka bayana muundo unaolenga kumpa kinga na viwango ili kutoa haki kwa watoto, kanuni za kuthibiti ajira kwa watoto pia zimepewa nguvu zaidi katika sheria hii. Vitendo vya utumikishaji wa watoto vinapingana na sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo si tu kwamba imefafanua haki za watoto katika mazingira mbalimbali, bali imeweka vifungu vinavyoainisha wajibu wa watendaji, wakiwemo wazazi katika kuwalinda na kuwajali watoto. Kifungu cha 9 cha sheria hiyo kinaainisha wajibu wa wazazi kwa watoto wao ingawa vipo vifungu vingine vinavyoashiria wajibu wa mzazi. Kifungu hiki ni lazima kitafsiriwe kulingana na wajibu unaotokana na haki za mtoto kwamba ana haki ya kuishi, kulindwa utu wake, heshima, mapumziko, uhuru, afya, elimu na malazi stahiki kutoka kwa wazazi wake" Amefafanua zaidi Mhe. Mzeru.

Katika hatua nyengine, amesema suala la ajira  kwa watoto ni jambo linalopigwa vita duniani kote, ili kuhakikisha kwamba jumuya ya kimataifa inafuata misingi na viwango vya kimataifa kuhusu ajira kwa watoto, ilitengenezwa mikataba kuweka bayana misimamo ya kimataifa. 

Amesema kuwa , mkataba wa kimataifa wa mwaka 1989 unaujulikana dunia kote,uliopitishwa na baraza kuu la umoja wa mataifa ambapo Tanzania ilisaini mkataba huu julai 10 1999.

Pia, amesema mkataba wa Afrika wa mwaka 1999 kuhusu haki na wajibu wa mtoto inasisitiza kutokomezwa kwa ajira mbaya ya watoto huku akisema licha ya mikataba hiyo lakini kuna mikataba  mingine miwili ambayo lengo lake ni kuweka misingi inayolenga kuondoa ajira kwa watoto. 

Amesema, nchi zinalizoridhia mikataba hiyo ikiwemo Tanzania zinawajibika kuhakikisha zinatekeleza wajibu huo na ni lazima ziweke misingi hii katika sheria za nchi zao, ili ziweze kuitekeleza kwa ufasaha zaidi huku akisema kuwa watoto wanaofanyishwa kazi  hususani wa watoto wa kike ndio wako katika hatari zaidi ya kubakwa, kupata mimba na kuolewa kwa nguvu kuingia katika ndoa za utotoni, ufikiaji wao wa elimu umekuwa duni. 

Aidha amesema , kunyimwa haki yao ya kushiriki katika masuala ya kuwaendeleza, ushiriki wa watoto wa rika zote na hasa watoto wa kike umekuwa duni.

"Nikiri kwamba upo  ukiukwaji wa haki za watoto, kuna kundi kubwa la watoto ambao ndiyo mustakabali wa Taifa wakiwa wamekosa matumaini, baadhi yao wanakosa fursa za elimu kutokana na wazazi kutothamini elimu, wengine wanatumikishwa kinyume cha sheria katika migodi yenye leseni na isiyokuwa na leseni, kutumikishwa katika mashamba makubwa, kufanya vibarua vya kubeba mizigo, kuchunga mifugo, na kazi za ndani hali ambayo inawaathiri kisaikoloji katika maisha yao huku  yatima, ambao idadi yao inazidi kuongezeka kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, wameachwa bila msaada" Ameongeza Mhe. Mzeru.

Aidha, amesema   kuna mambo kadhaa yanayoeleza sababu za wanafunzi kuwa na mazoea ya kuacha shule kwa watoto walio toka katika familia zenye rasilimali kidogo, tishio linatokana na sababu kama vile viwango vya watoto waliovunja sheria, viwango vya juu vya watoto waliopata mimba, wakiwa wadogo na kutegemea kiuchumi mzazi au wazazi wenye mapato ya chini.

Hata hivyo, amesema  zipo sababu nyengine za ukatili wa kijisni ambapo hili linatokana na familia au jamii zisizotilia maanani uwekezaji katika elimu na maendeleo ya watoto maskini hupata matokeo yasiyo mazuri kwani baadaye watoto hawa hukosa kazi na huwa na vipato vidogo, Viwango vikubwa zaidi vya kuzaa mapema na hatari zake kwa familia, afya na maisha bora kwa ujumla ndiyo mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa kwa kuwa elimu kutoka kiwango cha shule ya msingi hadi shule ya sekondari ina umuhimu mkuu maishani.

Mhe. Mzeru, amesema Watoto wanatoka katika kaya maskini hawapati huduma muhimu, hii inawafanya wakose kwenda shule kwa siku nyingi katika kila mwaka Pia, tafiti mbalimbali zinaeleza kwamba kuna uwezekano zaidi kwa watoto maskini kuteseka kwa njaa, uchovu, kukasirika ovyo, maumivu ya kichwa, maambukizi ya masikio, mafua na homa ambapo magonjwa hayo yana uwezo wa kumzuia mtoto au mwanafunzi kuelewa yale anayofunzwa darasani.

Pia amesema kuwa , maeneo yaliyoathiriwa sana na umaskini mara nyingi yanaweza kuwa na ukatili mwingibaadhi ya watoto wengine hawasomi vizuri darasani hasa wale wa kutoka jamii maskini katika maeneo yenye makazi duni na wengine wanakuwa wanakosa ari ya kusoma kutokana na kutokuwa na uhakika wa chakula nyumbani kwao.  

Hata hivyo, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine inapaswa kukomesha ajira kwa watoto.

Hata hivyo, Mhe. Mzeru,  ametoa wito kwa wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea, kuwatunza na kuwalinda watoto ambao ni Taifa la kesho kwa kutowatumikisha katika kazi ambazo haziendani na umri wao.

Mwisho amewaomba sana Wana CCM kwa kushirikiana na Serikali kuwa ni vyema sasa wakaweka nguvu za pamoja za kuhakikisha kwamba suala la ajira kwa Watoto na ukatili wa Kijinsia linakomeshwa tunavikomesha japo Serikali ya Tanzania inazo sheria nzuri zinazozuia ajira kwa watoto, ingawa kuna changamoto kwenye suala la usimamizi wa kutekeleza sheria hizo.



 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.