Header Ads

RC MWASSA AWATAKA VIONGOZI KUTATUA KERO ZA WANANCHI.





MKUU wa Mkoa wa  Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa, amewaagiza Viongozi  wa Halmashauri  kufanya ziara za kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi badala ya kusubiri viongozi wa Serikali ya mkoa ndio wazitatue changamoto za wananchi.

Ametoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi Kata ya Kihonda, uliofanyika Septemba 13/2022 katika eneo la Ofisi ya Kata ya Kihonda .


RC Mwassa, amesema  serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo lakini wananchi hawajui kinachoendelea kwasababu viongozi ambao wanapaswa kuwaeleza hawafanyi hivyo.

"Ni muhimu mno kufanya mikutano ya wananchi kusikiliza kero zao, wahamasisheni madiwani, makatibu tarafa wafanye ziara, mkoa wetu umekuwa ukipata fedha nyingi za miradi ya maendeleo  ni wajibu wetu kama viongozi kuzisimamia ili zilete tija katika maendeleo," Amesema RC Mwassa.

Aidha, amesema kuwa kusikiliza ni moja ya uwajibikaji bora kwa wananchi, hivyo kutofanya mikutano ya hadhara kwa wananchi kuna sababisha  kuibuka kwa kero nyingi ambazo kama ziara zingekuwa zinafanyika hali hiyo isingejitokeza.

Katika hatua nyengine, amepiga marufuku Watendaji wa Kata na Mitaa na wenyeviti wa Serikali za Mitaa  kutojihusisha na uuzaji wa ardhi, kwani kufanya hivyo kuna pelekea kuwa na mlundikano wa migogoro ya ardhi kila uchwao.


Hata hivyo, RC Mwassa, amewaagiza Viongozi wa Wilaya na Halmashauri  kwa kushirikiana na wataalam wa ardhi kufuatilia migogoro yote ya ardhi na kuipatia ufumbuzi na kuiweka kwenye 'data base'.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa,  amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa  kuwa yote aliyoyaagiza atayafanyia kazi kwa kushirikiana na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa.

RAS Mussa, amewataka Watumishi wa Umma kuhakikisha kila mtumishi awe na sheria ya Serikali za Mitaa ambayo sheria hiyo ndio inayoonesha majukumu yao kwa ujumla katika kuwatumikia wananchi.

"Mkasome sheria za Serikali za Mitaa, lakini kila mtumishi awe na Ilani ya CCM inayoelekeza mambo ya kufanya , pia tuangalie maelekezo ya mkoa yanataka nini , tujenge utamaduni wa kuwajibishana ili mifumo ifanye kazi , kwa kufanya haya tunaamini kabisa tutaweza kufikia viwango vya juu vya utendaji " Amesema RAS Mussa.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.