RC MWASA AWATAKA WANANCHI KUJIEPUSHA NA MATUMIZI YA MIFUKO YA PLASTIKI
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa,amewataka wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wafanyabiashara kujiepusha na matumizi ya mifuko ya Plastiki pamoja na mifuko mbadala isiyokidhi viwango vya ubora na sifa zilizowekwa na TBS.
Kauli hiyo ameitoa Septemba 17/2022 wakati wa mkutano wake na wafanyabiashara wa Manispaa ya Morogoro eneo la Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
" Ni wajibu wa Kila Mtanzania kutoa taarifa haraka kwa Mamlaka husika ,ikiwemo Ofisi yangu, Halmashauri husika na NEMC , pale mnapohisi au kuona mtu au kampuni yoyote inajihusisha na uzalishaji, uingizaji , usafirishaji , usambazaji , uhifadhi na matumizi ya mifuko ya Plastiki" Amesema RC Mwassa.
RC Mwassa, amewasihi wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa mifuko ya Plastiki isiyokidhi viwango ,kusalimsha wenyewe mifuko hiyo katika Ofisi za Halmashauri au Ofisi za NEMC kanda ndani ya muda wa siku 2 kuanzia Septemba 17/2022 kabla ya msako kupita.
Hata hivyo, ameziagiza Taasisi na Mamlaka zote zinazohusika na utekelezaji wa katazo la mifuko ya Plastiki ,kuanza mara moja ukaguzi wa maeneo mbalimbali yanayojihusisha na biashara ya mifuko mbadala na vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango au sifa zilizowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Mwisho, RC Mwassa, amevishukuru vyombo vya habari kwa kuunga mkono katika kampeni ya kuendeleza elimu ya kutokomeza mifuko mbadala na vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango na sifa zilizowekwa na TBS.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amewataka wananchi kuwa wazalendo na kuacha matumizi ya mifuko isiyo na viwango na ubora ambayo ina madhara katika ustawi wa maisha ya binadamu na mazingira yake.
Miongoni mwa sifa za Vifungashia vya plastiki ni viwe na anuani ya mzalishaji, alama ya urejelezaji ,viwe na TBS, viwe na unene usiopungua microns 30 (0.03mm) kwa upande mmoja au microns 60 (0.06mm) pande zote mbili.
Sifa za Mifuko Mbadala ni iwe na jina la mzalishaji, alama ya urejelezaji,iwe na uzito usiopungua GSM 70 (Gram per square meter), ioneshe uwezo wake wa kubeba (carry capacity) na iwe imethibitishwa na TBS.
Post a Comment