Header Ads

MEYA KIHANGA AKABIDHI MADAWATI 200 YALIYOJENGWA NA BARAZA LA MAENDELEO KATA YA KILAKALA.



MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amekabidhi madawati 200 yaliyogharimu Milioni 2 na laki 6  kwa shule 3 za Msingi  ikiwamo shule ya Mwande, Kigurunyembe na Kilakala yaliyotengenezwa  kupitia uvunaji wa  rasilimali ya miti yao chini ya usimamizi wa Baraza la Maendeleo la Kata ya Kilakala.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo, Mhe. Kihanga, ameupongeza Uongozi wa Kata ya Kilakala  chini ya Diwani  Mhe. Marco Kanga pamoja na wadau wote waliofanikisha utengenezaji  wa madawati hayo.

Mhe. Kihanga, amewataka waku wa shule hizo 3 ambao wamekabidhiwa madawati hayo  kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa vizuri ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kutumiwa na wanafunzi wengine hapo baadaye.

Kwa upande wa Katibu wa CCM  Wilaya ya Morogoro Mjini, Chifu Sylevester Yared, ameupongeza Uongozi wa Kata kwa hatua ya kuboresha elimu huku akisisitiza  kusimamia elimu kwani kipaumbele ni taaluma inayoweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya  elimu katika Taifa letu ambapo amesema  Serikali ya awamu ya Sita inafanya jitihada kubwa katika suala la kuboresha elimu kwa kujenga miundombinu mbalimbali.

Naye Diwani wa Kataya Kilakala, Mhe. Marco Kanga, amesema Shule za Msingi Kata ya Kilakala zilikuwa zinakabiliwa na uhaba wa madawati hivyo anaamini madawati hayo yatakidhi haja na kuondoa tatizo hilo.

" Nawashakuru wadau wote waliofanikisha ujenzi wa madawati haya, tunamshukuru Mkuu wetu wa Wilaya kwa ushirikiano wake , Mkurugenzi wa Manispaa, Mbunge wetu Mhe. Abood na wadau wote pamoja na waalimu waliojitolea fedha katika kufanikisha hili, sasa tunahamia katika shule za Sekondari ili tumalize sasa matatizo ya madawati katika shule zetu za Msingi na Sekindari" Amesema Mhe. Kanga.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.