Header Ads

DIWANI CHOMOKA ATAKA FAMILIA NA JAMII KUWATUNZA WAZEE





DIWANI wa Kata ya Mkundi ambaye ndiye mgeni rasmi katika maadhimiisho ya Siku ya Wazee Duniani Kata ya Mafiga, Mh. Seif Chomoka, amesema wazee wanapaswa kutunzwa na kwamba Serikali inawathamini sana kwani wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali katika hali ya uzee.

Kauli hiyo ameitoa Septemba 29/2022 katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro yaliyofanyika kwenye eneo la Kituo cha Afya Mafiga.

Akizungumza na Wazee waliojitokeza katika sherehe hiyo, Mhe. Chomoka, ameitaka jamii kuwajibika kwa kuwatunza  na  kutambua kuwa wazee ni tunu kubwa katika maisha hivyo wanapaswa kutunzwa badala ya kunyanyaswa.

Pamoja na hayo, Mhe. Chomoka,  amesema upande wa Halmashauri maboresho ya upatikanaji wa huduma kwa wazee yanaendelea kwa kuhakikisha zahanati, vituo vya afya na hospitali kunakuwa na dirisha la wazee  huku akiwashauri wazee hao kutumia vema fursa ya uwepo wa baraza la wazee kuainisha changamoto zao ili ziweze kushughulikiwa lakini pia kufanya mazoezi ya viungo ili kuwa na siha njema.


Akibainisha namna Serikali inavyowajali , Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, amewataka wauguzi wa afya kuhakikisha dirisha la wazee linasimamiwa ipasavyo ikiwamo upatikanaji wa huduma za afya  na huduma nyinginezo.

Mhe. Butabile, amesema Mafiga ina jumla ya wazee 307 ambapo wamekuwa wakishirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kijamii .

Mbali na hayo, maadhimisho hayo yameendaana sambamba na kukagua miradi ya maendeleo ikiwamo kufungua madarasa 3 mapya yaliyojengwa na fedha za Serikali kwa kushirikiana na michango ya wananchi.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.