MANISPAA YA MOROGORO YAPONGEZA BARAZA LA WAZEE BIGWA KWA MAANDALIZI MAZURI YA MAADHIMISHO.
MANISPAA ya Morogoro imepongeza maandalizi mazuri yaliyofanywa na Baraza la Wazee Kata ya Bigwa katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani.
Kauli hiyo , imetolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Caroline Sakaya, wakati wa maadhimisho hayo ngazi ya Kata yaliyofanyika Septemba 15/2022 Kata ya Bigwa.
Dr. Sakaya, amesema Kata ya Bigwa iwe mfano kwa mabaraza mengine kwani wameonesha mfano mzuri katika maandalizi yao.
Aidha, Dr. Sakaya, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha maisha ya wazee hapa nchini ili kuhakikisha wanapata huduma jumuishi na stahiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee kuwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Dr. Sakaya, amesema famila na jamii kwa ujumla wana wajibu na jukumu la kuwatunza wazee kwa kuwaheshimu na kutekeleza matakwa ya mahitaji yao kwani jukumu la kumtunza mzee linakwenda sambamba na kumhudumia pindi anapoumwa na anapokuwa mzima .
Diwani wa Kata ya Bigwa, Mhe. Merichior Mwamnyanyi, amesema atahakikisha kuwa anakuwa bega kwa bega na Baraza la Wazee wa Kata hiyo kwani lengo la Baraza hilo ni kuleta wazee pamoja katika mijadala mbalimbali na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Akitoa salamu kwa niaba ya Wazee wenzake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro, Mzee Rashid Zongo, ameushukuru Uongozi wa Manispaa na Serikali kwa ujumla kwa huduma wanazozipata na kumuomba Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya, chakula na malazi ili waweze kuishi kwa amani na furaha zaidi.
Sherehe za maadhimisho ya siku ya wazee itahusisha huduma mbalimbali kama vile wazee kupima presha, kisukari, tezi dume, huduma za msaada wa kisaikolojia na elimu kuhusu kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuhamasisha wazee na wananchi kupata chanjo.
Maadhimisho siku ya Wazee Duniani Manispaa ya Morogoro yatafanyika Septemba 24/2022 katika Kata ya Tungi yenye Kauli mbiu "Matumizi sahihi ya kidigitali kwa ustawi wa rika zote’’ pamoja na kupatiwa elimu na kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19.
Post a Comment