DIWANI CHUNGA ATAKA USHIRIKIANO WA WATENDAJI KULETA MABADILIKO
DIWANI wa Kata ya Mzinga,Mhe. Salum Chunga, amewataka Watendaji wa Kata ya Mzinga pamoja na wananchi wa Kata hiyo kushirikiana katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Kata hiyo.
Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni katika Mkutano wa Baraza la Maendeleo la Kata (BMK) Septemba 14/2022 wakati akipokea taarifa mbalimbali za utekelezaji .
Mhe. Chunga , amesema kuwa Watendaji wakishirikiana vyema na kuwa kitu kimoja kwa wakishirikiana vizuri wananchi watapata maendeleo kwa haraka zaidi.
“Mimi nitajitahidi kuwa mvumilivu maana ndio Kiongozi Mkuu wa Kata, lakini sitakuwa mvumilivu na mtu yoyote anayekwamisha au atakayekwenda kinyume na haya tunayoyapanga, kwani kwenda kinyume ni kuchelewesha maendeleo ya wananchi wetu " Amesema Mhe. Chunga.
Aidha, amewaomba Wenyeviti wa Mitaa kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Katika hatua nyengine, Mhe. Chunga, amewataka Watendaji pamoja na Wenyeviti wa Mitaa kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya afya iliyoboreshwa ya CHF ili wananchi wapate unafuu wa matibabu wanapofika katika vituo vya afya kufuata huduma.
Amesema kwa sasa changamoto iliyopo ni upande wa madarasa 3 ambayo yanahitaji kumaliziwa kwani upauaji na uwezekaji umefanyika.
Mbali na Shule lakini ameomba Serikali kuwaangalia kwa huruma hususani katika kumalizia ujenzi wa Majengo ya Zahanati yao ambayo kwa sasa yamefikia hatua nzuri bado upauaji na umaliziaji ili yaweze kutumika.
Amesema changamoto nyengine ni barabara , ambapo ameiomba Serikali kuweka nguvu katika kuboresha barabara kwani imekuwa ni changamoto hususani katika kipindi cha mvua.
Post a Comment