BODABODA MANISPAA MOROGORO WATOA TAMKO KALI MADEREVA WATAKAO JIHUSISHA NA MAANDAMANO.
Uongozi wa CHAWAPIMAMO, ukiwa katika picha ya pamoja Ofisini kwao mara baada ya mahojiano juu ya kupiga vikali maandamano kwa Vijana wa Bodaboda wanaotaka kutumiwa na baadhi ya Vyama vya Siasa kuvuruga amani.
CHAMA Cha Waendesha
Pikipiki Manispaa ya Morogoro (CHAWAPIMAMO)
,kimelaani na kupinga vikali maandamano
ya Madereva watakaotumika kufanya maandamano na kuvuruga amani ya nchi.
Akitoa tamko kwa niaba
ya Chama hicho, leo Novemba 03,2020 kwenye Ofisi za Chama hicho
kilichopo Kata ya Mji Mpya TTCL Manispaa ya Morogoro , Mwenyekiti CHAWAPIMAMO, Justine Mkoba, amesema umoja
wao umepinga njama zinazofanywa na baadhi
ya vyama vya Siasa ya kuwatumia madereva hao na
kusisitiza kuwa njama hizo hazitafanikiwa katika Manispaa hiyo.
Amesema kinachotaka
kufanyika sasa baada ya uchaguzi kukamilika na
matokeo kutangazwa kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi
na Mamlaka halali ni vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo
amesema halikubaliki badala yake amewasihi wananchi wafanye
kazi ili kuiletea nchi yetu maendeleo zaidi
katika awamu ya sasa.
“Tumejipanga kukabiliana
na uhuni wowote ambao umepangwa kufanywa kwenye kipindi hiki na
baadhi ya wahuni wachache wasioitakia mema nchi yetu,
tunaomba vyombo vya ulinzi visimamie hili kikamilifu na
sisi tupo nyuma yao, yule ambaye atafanya maandamano hayo na tukagundua ni
mwanachama wetu tutamfuta Uanachama na atachukuliwa hatua kali za sheria ” Amesema
Mkoba.
Amemwomba Mhe. Rais, John
Pombe Joseph Magufuli, kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania ili
itoke kwenye Uchumi wa Kati hadi Uchumi wa juu kabisa na
hatimaye kuboresha maisha ya watanzania wote.
Kwa upande wa Katibu wa
CHAWAPIMAMO, Juma Bega, amewaonya madereva wa Bodaboda ambao
kwa namna moja au nyingine watatumika katika kuvunja Sheria za nchi
kwa kupanga njama za kufanya maandamano yasiyo ya amani
ambayo hayana kibali kutoka Jeshi la Polisi.
Bega, ameongeza kuwa
wananchi wameamua kuwachagua viongozi wanao wapenda hivyo hakuna sababu ya watu
kuandaa njama za kupinga matokeo ya uchaguzi.
Naye Naibu Katibu wa Chama
hicho, Nurani Ismail, ameipongeza Serikali kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa
Mwaka huu kwa uwazi ambao umeweza kufuata taratibu zote na kutoa
matokeo kwa wakati.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi
Nchini (NEC), Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John
Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5 Mwaka huu kwenye uwanja
wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Post a Comment