Header Ads

WASIMAMIZI MTIHANI WA UPIMAJI DARASA LA NNE MANISPAA YA MOROGORO WATAKIWA KUTUNZA SIRI NA KUWA WAAMINIFU.

Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Pili Kitwana, akifungua semina.

Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro, Chausiku Masegenya, akizungumza na Wasimamizi wa mtihani kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya ufunguzi wa Semina.



Afisa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Bigambo Thomas, akizungumza na wasimamizi wa mtihani wa kujipima darasa la Nne .






WASIMAMIZI wa Mtihani wa upimaji darasa la Nne (SFNA-2020) , Manispaa ya Morogoro wametakiwa kutekeleza wajibu wa kusimamia mtihani huo kwa uaminifu mkubwa wa kutunza siri kwa taarifa zozote wanazozifahamu.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Pili Kitwana, Novemba 19/2020 , wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kwa wasimamizi wa mtihani wa upimaji darasa la Nne kwenye Ukumbi wa St. Francis Kihonda Maghorofani.

Kitwana,amesema kuwa kama ilivyo  kawaida, kila mwaka  taarifa za vitendo vya udanganyifu  zimekuwa zikiripotiwa katika maeneo mbalimbali ambako mitihani inakofanyika, jambo linaloweza kusababisha wanafunzi kufutiwa matokeo na wahusika wa vitendo hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, amesema kuwa katika semina hiyo watajifunza mbinu mbali mbali zitakazosaidia kuzuia watahiniwa kuiba majibu ambayo yatapelekea kupata alama za juu ambazo si halali kwao.

Amesisitiza wasimamizi kuhakikisha wanawakagua watahiniwa kikamilifu kabla hawajaingia katika vyumba vya mitihani na wawe makini wakati wote mtihani unapokuwa ukiendelea.

“Kuna watu wenye nia mbaya wanaweza kuwarubuni ili msitekeleze majikumu yenu vizuri ikiwa ni pamoja na kuhatarisha usalama wa mtihani huu, niwaase kuwa hamuingii kwenye ushawishi wowote utakaosababisha kuharibika kwa Mtihani huu na wewe kuingia katika matatizo makubwa yatakayopelekea hatua kazi za kisheria kuchukuliwa dhidi yako” Amesema Kitwana.

Amesema Manispaa ya Morogoro ina jumla ya shule za msingi 94 zitakazofanya mtihani wa upimaji darasa la Nne (SFNA 2020), kati ya hizo shule 64 ni za Serikali na shule 30 zisizo za Serikali.

Hata hivyo, amesema jumla ya wanafunzi 11269 wakiwemo wavulana 5786 na wasichana 5483 wanatarajia kufanya Mtihani wa Upimaji darasa la Nne.

Pia amesema kuna jumla ya mikondo 398 ya mfumo wa Kiswahili na 85 ya mfumo wa Kiingereza , hivyo kufanya idadi ya mikondo yote kuwa 483.

Mwisho, amewatakia mafanikio mema katika kazi hiyo huku wakizingatia maelekezo yote yatakayotolewa na wakufunzi wa semina hiyo katika kufanikisha zoezi hilo kwa usalama.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.