Waliopata mafunzo ya jeshi la Akiba (Mgambo) Wilaya ya Morogoro watakiwa kuwa wazalendo.
MKUU wa Wilaya ya
Morogoro, Bakari Msulwa, amewaasa Vijana
kuwa wazalendo wa nchi yao kwa kuacha kujiingiza katika viashiria vya uvunjifu
wa amani ili kusaidia kuepukana na migogoro itakayopelekea uvunjifu wa Amani.
Hayo
ameyasema leo Novemba 25/2020 wakati kufunga rasmi mafunzo hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa mpira wa miguu wa Jamhuri.
Msulwa, amesema kuwa
itakuwa ni fedheha kwa taifa ikibainika kuwa vijana hao waliopikwa kwa misingi
ya uzalendo wameshiriki katika matukio ya ujangili na migomo isiyo na tija au kutumika kisiasa.
Katika
hatua nyengine, amewapongeza wahitimu wote na kuwasihi kuyatumia mafunzo hayo
kama chachu ya kujiletea maendeleo na kuhakikisha kuwa wanailinda jamii
inayowazunguka.
Aidha, amewaahidi kuwa Serikali ipo nao bega
kwa bega na ndiyo maana imetumia gharama kubwa kuwapatia mafunzo hayo.
Hata
hivyo, ametumia fursa hiyo kuyaomba makampuni binafsi ya ulinzi kuwatumia
vijana hao wenye mafunzo ya kijeshi kwa shughuli zao za ulinzi.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwaasa vijana wilayani humo kuwa inapotokea fursa
kama hiyo wajitokeze kwa wingi na wasikatishwe tamaa kwani Serikali inatumia
gharama kubwa kufanikisha mafunzo hayo.
"Vijana wangu najua mmepitia vikwazo vingi na ninajua mlikatishwa tamaa
maana wapo mabingwa wa kukatisha watu tamaa lakini mmevuka salama na leo
mnahitimu, basi mafunzo haya yawe na tija katika maisha yenu binafsi na jamii
inayowazunguka". Amesema DC Msulwa.
Mafunzo hayo ya miezi 4 yamejumuisha jumla
ya Vijana 200 chini ya usimamizi wa
Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Morogoro.
Post a Comment