Header Ads

WANANCHI MANISPAA MOROGORO WASHAURIWA KUJENGA NA KUTUMIA VYOO BORA.

 

Kaimu Afisa afya Manispaa ya Morogoro, Nobert Bilaba, akitoa elimu kwa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mafisa 'A' Kata ya Mwembesongo juu ya matumizi sahihi ya choo.

Afisa Mazingira, Alex Romani, akitoa zawadi kwa mwanafunzi aliyejibu vizuri swali kuhusu matumizi bora ya choo.

       

Baadhi ya Watendaji wakionekana na sura za furaha wakati wa kilele cha siku ya choo na usafi wa Mazingira.

      

Kaimu Afisa afya Manispaa ya Morogoro, Nobert Bilaba,akiwafundisha mwanfunzi jinsi ya kunawa mikono wakati wa kutoka chooni.

   


Choo cha zamani Shule ya Msingi Mafisa 'A' 

Choo kipya cha Shule ya Msingi Mafisa 'A' ambacho kipo katika hatua za mwisho kumalizika .


WANANCHI wa Halimashauri ya Manispaa ya Morogoro,  wameshauriwa kujenga  vyoo bora na kuboresha usafi wa mazingira.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Afisa Afya Manispaa ya Morogoro, Nobert Bilaba , wakati akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi bora ya vyoo katika Shule ya Msingi Mwembesongo ambapo maadhimisho ya kilele hicho yalifanyika.

 

Nobert,  ameeleza sifa ya choo bora ni kuwa na sakafu safi inayo safishika vizuri,kuta imara zinazotunza faragha, paa rafiki,hakiruhusu mazalia ya wadudu ,sifa nyingine ni kuwa na maji tiririka maeneo ya chooni na sabuni ya kunawa baada ya kujisaidia.

Amesema wa vyoo bora na uboreshaji wa mazingira utasaidia kupunguza magonjwa  ya matumbo kwenye jamii.

Amezitaka kamati za kampeni za usafi  wa mazingira zilizoundwa kila Mtaa  kuhakikisha zinaendelea kuhamasisha wananchi kujenga vyoo bora na kuvitumia kwa usahihi katika makazi yao.

Ametaja magonjwa yanayotishia uhai wa binadamu yanayo sababisha na utupaji wa kinyesi hovyo kuwa ni minyoo,kichocho tumbo,homa ya matumbo kama vile kuhara damu na kawaida ambayo yanaweza kuepukika kwa kuzingatia kanuni za afya na matumizi bora ya vyoo.

“ujenzi wa nyumba bora na za kisasa uende sambamba na ujenzi wa vyoo bora, baadhi ya watu  hawana sehemu maalumu ya kujisaidia wanatumia vyoo vya mtaani,  vichakani au sehemu nyingine zilizo karibu na nyumba zao, hii ni kwasababu ya kutokuwa na mwamko wa kujenga vyoo au kuwa na mazoea ambayo yameshajengeka na kuona choo hakina umuhimu, jambo linalowafanya watu kujisaidia kwenye vyanzo vya maji na kusababisha uchafunzi wa mazingira” Amesema Nobert .

Naye Afisa Mazingira Alex Roman, amesema kwa  kuona  umuhimu wa kuwepo kwa vyoo bora, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya na mazingira wamekuwa na kampeni mbalimbali i ili waweze kusaidiana katika kuwapa watu elimu kuhusu matumizi sahihi ya vyoo.

Sambamba na hilo, Romani,amewataka  watendaji wa Kata na Mitaa  kutimiza wajibu na kusimamia sheria ndogo ili wananchi wawe na
vyoo bora.

Kwa Upande wa Afisa Mtendaji Kata ya Mwembesongo,Sikudhani Jasson, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, kwa kusikiliza kilio chao na kuwapatia choo cha kisasa Shule ya Msingi Mafisa ‘A’.

“Awali tulikuwa na changamoto sana ya choo kwa wanafunzi wetu, tulikuwa tunatumia choo ambacho sio bora sasa Mkurugenzi wetu ameliona hili, tunashukuru wakati tunasherekea kilele cha siku ya choo duniani na usafi wa mazingira huku tukiwa na choo kipya cha kisasa ambacho kipi katika hatua za mwisho  kukamilika” Amesema Sikudhani.

Mbali na shule, lakini Maafisa hao wa afya na Mazingira Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Watendaji wa Mitaa Kata ya Mwembesongo walifanya ziara ya kutembea katika Mitaa kwa ajili ya kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya Choo . 


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.