Header Ads

**8/

Afisa Maendeleo ya Jamii , Mwanitu Sembogo, (kushoto) akipokea risala kutoka kwa Mkuu wa Kituo cha kulelea Yatima Mgolole, Bi Evarista Bunga, wakati wa sherehe ya kumkumbuka Mtakatifu Vicent iliyofanyika Septemba 27,2020 kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mgolole.


HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imewapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kusaidia Vituo vya Watoto yatima katika kuhakikisha wanapata huduma stahiki.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii, Mwanitu Sembogo, akimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa  ya Morogoro katika sherehe iliyoandaliwa na Makao ya kulelea Watoto ya Mgolole  ya kumkumbuka Mtakatifu Vicent kwa ajili ya matendo yake aliyokuwa akiyafanya katika kuwasaidia Watoto yatima,  Wazee na watu wasiojiweza wenye mahitaji maalumu.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Sembogo, ameiomba jamii kuendelea kuelekeza macho katika kusaidia Vituo kama hivyo ili kuvipa uwezo wa kulea Watoto na kupunguza Watoto wanaoteseka kwa kukosa msaada.


""Tuna shukuru sana Uongozi wa Mgolole kwa hatua mliyofikia licha ya kuwepo kwa changamoto zinazowakabili lakini kiukweli mmekuwa msaada mkubwa sana kwa jamii , mnatusaidia sana Serikali katika kupunuza wimbi la Watoto mitaani, lakini hii misaada yote mnayoiona leo hapa kutoka kwa wadau mbalimbali wanatoa  ili watoto hawa nao wajione kama sehemu ya jamii na waweze kutimiza ndoto zao ikiwemo za kupata elimu bila vikwazo pamoja na kusihi kwa matumaini kama wanavyoishi watoto wengine mitaani wakiwa na Wazazi na walezi wao, niwaombe wadau tuendelee kumulika kwa jicho pana Vituo vyetu hivi ili tuzuie wimbi la Watoto mitaani "Amesema Sembogo.

Amesema  kuwa ni vema  wanajamii wakaendelea kujitolea kwa watoto kama hao ambao wanahitaji msaada wakati wote ukizingatia kuwa hawana wazazi isipokuwa wazazi wao ni jamii inayowazunguka.

Aidha, amesema Manispaa ya Morogoro  itaendelea kutoa ushirikiano na Vituo vya kulelea Watoto yatima katika kuhakikisha kwamba Watoto hao wanapatiwa huduma nzuri huku akitoa  pongezi kwa mlezi wa kituo hicho na kumshukuru  kwa juhudi anazozifanya   kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao na malezi kwa ujumla.

Mwisho amesema ni vizuri  kwa  jamii ikajiwekea utaratibu kuwafikia watoto hao na wengine wenye hali kama hii na kuwasaidia kwa kadiri itakavyowezakana ili nao hapo baadae waweze kushiriki katika ujenzi wa Taifa katika sekta mbalimbali kama watumishi na wataalamu.

Naye Mkuu wa Kituo cha Watoto yatima Mgolole, Bi. Maria Evarista Bunga, amewashukuru wageni wote  kwa ujio huo  na kwa vitu ambavyo wamevitoa  kwa watoto hao  ambao ni yatima ambao wanahitaji kufarijiwa.

"Hakika  mmesaidia kwa mchango mkubwa na  niwakaribishe mara kwa mara kuja kuwatembelea na kuona maendeleo ya watoto hawa.""Amesema Bi. Bunga.


Katika hatua nyengine, mmoja wa wananchi waliofika katika Sherehe hiyo, Marco Kanga, ameshauri kuwa katika kuhakikisha  watoto hao wanakuwa na afya nzuri ni vyema Serikali na wadau wengine wakachukua jitihada za makusudi za kuwakatia Watoto hao bima ili ziweze kuwasaidia kupata matibabu.

Mgolole ni miongoni mwa Vituo vya Kulelea Watoto yatima ambapo kilianzishwa mwaka 1937 na Baba Askofu Bernard Hilhorst Holanzi ambaye ndiye alikuwa Askofu wa Jimbo la Katoliki la Morogoro na mwakilishi wa Shirika la Masista wa Moyo safi wa Maria wea Morogoro ambao ndio walezi wakuu wa Watoto yatima.






No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.