MANISPAA YA MOROGORO YATOA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA VIKUNDI VYA WAAWAKE , VIJANA NA WATU WENYE LEMAVU.
HALMASHAURI ya Manispaa ya
Morogoro leo Septemba 16,2020 imetoa
mafunzo kwa ajili ya vikundi vya
wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika ukumbi wa Mikutano
wa Manispaa.
Akizungumza na Waandishi
wa Habari, Afisa Maendeleo ya Jamii, Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe,
amesema lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea
uwezo wa kutumia vema na kurejesha mikopo ambayo Halmashauri inatoa asilimia 10
ya mapato yake kwa ajili ya kuviwezesha Vikundi hivyo kiuchumi.
Aidha, Mwanakatwe, amesema
Manispaa inatarajia kutoa Shilingi Milioni 214 laki 9 ya fedha zilizosalia za
mwaka wa fedha wa 2019/2020 ili kuviwezesha vikundi hivyo kujikwamua kiuchumi,
kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira kwa kujihusisha na shughuli
mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya Maisha yao na Manispaa kwa
ujumla.
Mwanakatwe, amesema kuwa
mikopo inayotolewa ina lengo la kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi
hivyo ni vyema wakatumia fursa ya kuchukua mikopo na kuitumia kikamilifu ili
waweze kurejesha marejesho kwa wakati.
Miongoni mwa mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na kuwafundisha
na kuwaelekeza jinsi ya kutumia mikopo hiyo kama ilivyokusudiwa na kujua namna
ya kutafuta masoko katika biashara zao, uandaaji wa mipango ya biashara,
uwekaji wa kumbukumbu, usimamizi na uendeshaji wa vikundi, sheria na kanuni za
mikopo, pamoja na kufahamu namna ya
uwekaji wa akiba.
Mwisho, amevitaka vikundi vyote kuwa mabalozi wazuri
kwa wananchi wengine ambao bado hawana muamko wa mikopo ya wanawake, vijana na
watu wenye ulemavu ambayo haina riba na kuendelea kuwasisitiza wanavikundi wote
waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili
kupata nafasi ya kukopesheka zaidi na kutoa fursa kwa vikundi vingine kuweza
kupata mikopo.
Post a Comment